1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yamtimua kocha Tuchel

30 Mei 2017

Kocha wa miamba wa soka wa Ujerumani Borussia Dortmund Thomas Tuchel ameyaacha majukumu yake kama kocha na haya yamethibitishwa na klabu hiyo.

https://p.dw.com/p/2dqhv
Borussia Dortmund BVB - Hamburger SV HSV
Kocha wa zamani wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel Picha: picture alliance/dpa/S.Matzke

Klabu hiyo lakini imekanusha kwamba kuondoka kwake kumetokana na mgogoro wa hadharani uliokuwepo baina ya Tuchel na afisa mkuu mtendaji wa klabu hiyo.

"Tunamshukuru Thomas Tuchel na makocha wake wasaidizi kwa kazi yao iliyoleta ufanisi BVB,"ilisema taarifa ya klabu hiyo ikiongeza, "sababu ya kuondoka kwake bila shaka sio kutoelewana kwa watu wawili."

Uhusiano baina ya Tuchel na afisa mkuu mtendaji Hans-Joachim Watzke umekuwa mbaya, tangu shambulizi la bomu katika basi la timu ya Dortmund Aprili 11.

Tuchel alikuwa amelalama kwamba yeye na wachezaji wake hawakushauriwa kuhusiana na uamuzi wa kuendelea kucheza mechi yao dhidi ya Monaco katika ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya, chini ya saa 24 baada ya tukio hilo. Lakini Watzke alikanusha madai hayo na kusema kauli hiyo ilimghadhabisha.

DFB Pokal ndilo lililokuwa taji la kwanza la Tuchel Dortmund

Katika taarifa Dortmund imesema haitotoa maelezo zaidi kuhusiana na suala hilo la kuondoka kwa kocha huyo.

Huku akiwa alikuwa amesalia na mwaka mmoja katika mkataba wake na Dortmund, Tuchel sasa atalipwa Yuro milioni 2.5 kama ada ya kuondoka hapo Signal Iduna Park. Kuondoka kwake kunakuja siku tatu tu baada ya Dortmund kuebuka mabingwa wa kombe la Ujerumani DFB Pokal baada ya kuilaza Eintracht Frankfurt 2-1.

Dortmund Pokalfeier Autokorso
Tuchel wakati Dortmund wakisherehekea ushindi wa DFB Pokal katika mitaa ya mji huoPicha: Reuters/I. Fassbender

Hilo ndilo lililokuwa taji la kwanza la Tuchel katika miaka miwili aliyokuwa kocha wa klabu hiyo na aliandika katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter, "nashukuru kwa miaka miwili mizuri yenye furaha. Nasikitika kwamba haitoendelea."

Ametimuliwa pia licha ya kuiongoza klabu hiyo kumaliza ya tatu katika msimamo wa Bundelisga na kujikatia tiketi ya moja kwa moja kushiriki ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya msimu ujao.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE

Mhariri: Bruce Amani