1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yaanza vyema Champions League

Josephat Nyiro Charo19 Septemba 2012

Robert Lewandowsky aliipatia Borussia Dortmund ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ajax Amsterdam katika mchuano wao wa kwanza wa Champions League uliochezwa jana (18.09.2012) mjini Dortmund.

https://p.dw.com/p/16BFv
Dortmunds Marco Reus (L) and Mario Goetze are seen prior the UEFA Champions League group D soccer match Borussia Dortmund vs. Ajax Amsterdam at BVB stadium in Dortmund, Germany, 18 September 2012. Photo: Marius Becker dpa/lnw
UEFA Champions League Borussia Dortmund gegen Ajax AmsterdamPicha: picture alliance/dpa

Mabingwa watetezi wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga, wakijizatiti kuwa na nafasi kubwa katika kundi D ambalo limeelezwa kuwa kundi gumu kabisa la kifo katika michuano ya msimu huu, walitolewa kijasho na Ajax kwa muda mrefu wa mechi yao na kushuhudia mlinzi wao Matt Hummels akikosa mkwaju wa penalti dakika ya 58.

Mario Goetze alifanyiwa madhambi na Ricardo van Rhijn na refa akapiga kipyenga kuipa fursa Dortmund kuongoza mechi hiyo, lakini kipa wa Ajax, Kenneth Vermeer, alikuwa na kazi rahisi kabisa kuuzuia mkwaju wa Hummels uliokuwa dhaifu. Lewandowsky ambaye alipoteza nafasi kadhaa za kufunga magoli, alipata mwanya dakika tatu kabla mechi kumalizika na kuutikisa wavu wa Ajax dakika ya 87 ya mpambano huo.

Kocha wa Dortmund, Juergen Klopp amesema mechi hiyo ilikuwa ya kusisimua na ngumu. "Tulilinda lango letu vyema muda wa zaidi ya dakika 90 na kutengeneza nafasi za kufunga mabao. Ilikuwa changamoto kubwa kuwa na uvumilivu. Timu hii imekuwa ikiendelea kuimarika vizuri kwa muda sasa na tunaendelea kufanya hivyo. Nimeridhika," aliongeza kusema kocha huyo.

Borussia Dortmund's coach Juergen Klopp reacts after the German first division Bundesliga soccer match against Bayer Leverkusen in Dortmund September 15, 2012. Dortmund won the match 3-0. REUTERS/Ina Fassbender (GERMANY - Tags: SPORT SOCCER) DFL RULES TO LIMIT THE ONLINE USAGE DURING MATCH TIME TO 15 PICTURES PER GAME. IMAGE SEQUENCES TO SIMULATE VIDEO IS NOT ALLOWED AT ANY TIME. FOR FURTHER QUERIES PLEASE CONTACT DFL DIRECTLY AT + 49 69 650050
Kocha wa Dortmund, Jürgen KloppPicha: Reuters

Kwa upande wake kocha wa Ajax Amsteredam, Frank de Boer, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amewaambia vijana wake wanaweza kujivunia mechi waliyocheza. Tulishindwa kufunga kwanza na kuongoza mechi hiyo. Hatuwezi kuwa na nafasi kama hizo na tusizitumie. Sio dhidi ya timu kama Dortmund." akasema kocha huyo.

Real Madrid yaishangaza Man City

Kwenye mechi nyengine ya kundi D, Real Madrid ya Uhispania iliibuka kidedea baada ya kuwachapa mabingwa wa ligi ya Premier, Manchester City mabao 3-2 uwanjani Santiago Bernabeu mjini Madrid. Edin Dzeko aliifungia Man City bao la kwanza dakika ya 22 lakini Real ikasawazisha kupitia Marcello dakika sita baadaye.

Aleksander Kolarov aliifungia Man City bao la pili dakika ya 86 na kukaribia kuipatia ushindi wa kihistoria timu yake dhidi ya Real, hadi pale Karim Benzema na Christiano Ronaldo walipoufumania wavu wa City dakika ya 87 na 90 ya mtanange huo.

Real Madrid's coach Jose Mourinho waits for the start of their Spanish King's Cup quarter-final second leg "El Clasico" soccer match against Barcelona at Nou Camp stadium in Barcelona January 25, 2012. REUTERS/Albert Gea (SPAIN - Tags: SPORT SOCCER HEADSHOT)
Jose MourinhoPicha: REUTERS

Kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho, amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana kama wanyama kukomboa na kushinda mechi hiyo. Kocha wa Man City, Roberto Manchini kwa upande wake amesema hali ni ngumu kwa kuwa walikaribia kuishinda Real mabao 2-1 zikiwa zimesalia dakika nne tu kabla mchezo kumalizika.

Real Madrid ina miadi na Ajax Amsterdam Oktoba 3 wakati Borussia Dortmund itakapomenyana na Manchester City.

Michuano mingine

Kwenye mechi za kundi B Schalke 04 ya Ujerumani iliishinda Olympiakos ya Ugiriki mabao 2-1, huku Arsenal London ikiishinda Montpellier mabao 2-1.

Kwenye kundi A, Paris Saint Germain iliichapa Dynamo Kiev mabao 4-1. FC Porto iliishinda Dinamo Zagreb mabao 2-0.

Na kwenye kundi C, AC Milan ilitoka sare tasa dhidi ya Anderlecht nyumbani, huku Malaga ikiinyoa bila maji Zenit St Petersburg mabao 3-0.

Mwandishi: Josephat Charo/APE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman