1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donad Trump adaiwa kuwasaidia wazazi wake kukwepa kodi

3 Oktoba 2018

Gazeti la Marekani la New York Times limeripoti rais wa nchi hiyo Donald Trump amejihusisha na udanganyifu wa kodi ambapo yeye na ndugu zake wanadaiwa kuwasaidia wazazi wao kukwepa kodi ya mamilioni ya dola.

https://p.dw.com/p/35uZ6
USA Trump Rede in Wheeling
Picha: picture-alliance/Zumapress/B. Cahn

Uchunguzi wa Gazeti hilo maarufu nchini Marekani New York Times ambao Ikulu ya White House, imesema unapotosha, umeonyesha Trump anapokea kwa sasa dola milioni 413 kutoka kwa biashara ya babaake ya majumba au mali zisizohamishika.

Gazeti hilo la Times likinukuu nyaraka kadhaa za mrejesho wa kodi pamoja na rekodi za kifedha, limesema utajiri alioupata Trump ni kwaajili ya kuwasaidia wazazi wake kukwepa kodi baada ya kuanzisha kampuni hewa pamoja na ndugu zake na kuficha mamilioni ya dola wakidai ni zawadi kutoka kwa wazazi wao.

Sarah Sanders Trump PK Sprecherin
Msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders Picha: picture-alliance/dpa/M. Brochstein

Trump alijisifia katika kampeni zake za uchaguzi wa urais kama mtu aliejijenga katika biashara hiyo ya majumba.

Alisema alianza kupitia mkopo kidogo aliopokea kutoka kwa babaake mfanyabiashara Fred Trump.

Kwa upande wake msemaji wa ikulu ya White House Sarah Sanders ameitaja ripoti ya Gazeti la New York times kuwa ya kupotosha huku wakili wa Trump Charles Harder akisema Rais Trump hajahusika kivyovyote na suala hilo.

Harder amesema masuala hayo yalishughulikiwa na watu wengine katika familia ya Trump ambao hawakuwa na ujuzi wowote na kutegemea wataalamu walio na leseni kuhakikisha wanafuata sheria.

Tayari uchunguzi umeanzishwa dhidi ya madai ya ukwepaji kodi

Huku hayo yakiarifiwa meya wa mji wa New York Bill de Blasio amesema katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter hapo jana jioni kwamba, ameielekeza idara ya fedha ya mji huo kuanzisha haraka uchunguzi wa ukwepaji kodi na kufanya kazi na serikali ya jimbo hilo kuhakikisha iwapo kodi zilizohitajika zililipwa.

Pressekonferenz Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: picture alliance/Zumapress

Nae James Gazzale, msemaji wa idara ya kodi na fedha ya jiji la New York awali alisema idara yake inaangalia kwa makini ripoti ya Gazeti la New York Times na wanaangalia njia za kuanzisha uchunguzi.

Gazeti hilo  maarufu nchini Marekani likiwanukuu wataalamu wa kodi, limeripoti kwamba haijawa wazi iwapo Trump atakabiliwa na mashtakaa ya uhalifu kwasababu matendo hayo yalikuwa yamepitwa na sheria ya ukomo. Gazeti la New York Times limesema hakuna ukomo wa sheria katika masuala ya faini za kiraia na udanganyifu wa kodi.

Gazeti hilo limesema ripoti yake imeandikwa kutokana na uchunguzi wa Nyaraka za kodi zaidi ya 200 kutoka kwa babaake Trump,  Fred Trump, kampuni zake na baadhi ya washirika wa Trump pamoja na watu wake wa karibu.

Muandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga