1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki inaomboleza maafa yaliyotokea Ankara

11 Oktoba 2015

Uchunguzi wa Uturuki kwa miripuko iliyouwa watu 128 nchini humo unaelekezwa kwa kundi la Dola la Kiislamu ambalo linatuhumiwa kuwa na mkono wake wakati upinzani ukimlaumu Rais Tayyip Erdogan kwa kuchochea shambulio hilo.

https://p.dw.com/p/1GmQo
Maadamano ya maombolezo ya miripuko ya Ankara. (11.10.2015)
Maadamano ya maombolezo ya miripuko ya Ankara. (11.10.2015)Picha: Reuters/U. Bektas

Serikali imesisitiza kwamba licha ya kutanda kwa hofu kutokana na shambulio hilo dhidi ya wanaharakati wa Kikurdi na makundi ya kiraia uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba Mosi utafanyika kama kawaida.

Maelfu ya watu wameandamana Jumapili karibu na eneo la shambulio hilo la Jumamosi kwenye kituo cha reli mjini Ankara wengi wakimshutumu Erdogan kwa kuchochea sera za utaifa kwa kuendesha kampeni za kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi madai ambayo serikali ya Uturuki inayakanusha.

Umati mkubwa uliokuwa umekusanyika katika uwanja wa Sihhiye ulikuwa ukipiga mayowe "Erdogan Muuaji"," "polisi wauwaji " lakini polisi wakiwa na magari ya maji ya kuwasha waliwadhibiti wasielekee kwenye kitongoji chenye majengo ya bunge na serikali.

Shambulio la Jumamosi limelishtuwa taifa la Uturuki lililokumbwa na kuibuka upya kwa harakati za wanamgambo wa chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi cha PKK katika eneo la kusini mashariki mwa nchi hiyo na kuenea kwa vita kutoka Syria.

Washukiwa wakuu Dola la Kiislamu

Duru mbili kuu za usalama zimesema alama za mwanzo zimeonyesha Dola la Kiislamu linahusika na miripuko hiyo ya Ankara na kwamba inafanana sana na shambulio la kujitowa muhanga la mwezi wa Julai katika mji wa Suruc karibu na mpaka wa Syria ambalo pia kundi hilo la Waislamu wa itikadi kali linalaumiwa kuhusika nalo.

Waandamanaji wakibeba picha za wahanga wa miripuko ya Ankara. (11.10.2015)
Waandamanaji wakibeba picha za wahanga wa miripuko ya Ankara. (11.10.2015)Picha: Reuters/U. Bektas

Duru hizo zimeliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba ishara zote zinadokeza kwamba Kundi la Dola la Kiislamu (IS) limefanya shambulio hilo na kwamba uchunguzi wao moja kwa moja unalilenga kundi hilo.

Ni rahisi kwa wanamgambo wa kundi hilo la IS lenye kushikilia sehemu kubwa ya Syria kujipenyeza Uturuki ambapo wanaishi wakimbizi milioni mbili wa Syria.Lakini kundi hilo ambalo sio kawaida kujinata kwa mashambulizi yake halikudai kuhusika na mripuko wa Suruc na hadi sasa halikusema iwapo limehusika na shambulio hilo la Ankara.

Shambulio baya kabisa

Taarifa ya serikali imesema watu 508 wamejeruhiwa katika miripuko hiyo 160 bado wangalipo hospitali na 65 wako katika vyumba vya watu mahututi katika hospitali 19.Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu ametangaza siku tatu za maombolezo ya taifa ambapo bendera zinapepea nusu mlingoti nchini kote.

Maadamano ya maombolezo ya miripuko ya Ankara. (11.10.2015)
Maadamano ya maombolezo ya miripuko ya Ankara. (11.10.2015)Picha: Reuters/U. Bektas

Rais Tayip Recep Erdogan ambaye umma ulioandamana umeitaka serikali yake iwajinike kwa kujiuzulu mwenyewe binafsi amelaani shambulio hilo katika taarifa kwa kuliita kuwa la "uovu mkubwa" na amefuta ziara yake Turkmenstan lakini bado hakulizungumzia hadharani shambulio hilo.

Idadi ya vifo vya shambulio hilo imepindukia ile ya mirupuko mwili ya mwezi wa Mei mwaka 2013 ambapo watu hamsini waliuwawa huko Reyhanli karibu na mpaka wa Syria na kufanya shambulio hilo la Ankara kuwa baya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Jamhuri ya Uturuki.

Wakati wasi wasi wa kimataifa ukiongezeka kuhusiana na ukosefu wa utulivu katika taifa hilo muhimu mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Rais Barack Omaba wa Marekani ametuma salamua za rambi rambi na mshikamano kwa Erdogan katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/Reuters

Mhariri : Isaac Gamba