Dk. Shein njia nyeupe Zanzibar
21 Machi 2016Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar CUF na mshirika wake Chadema hawakushiriki uchaguzi huo wakidai kuwa ni kinyume na sheria za uchaguzi na katiba ya Zanzibar. Tume ya uchaguzi ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa Oktoba ambao chama cha CUF kinaamini kilishinda.
Naibu Katibu mkuu wa CUF kwa upande wa Zanzibar Nassor Mazrui, alisema kuwa chama chake hakikushiriki uchaguzi huo kwa sababu wanachama wake wanaamini uchaguzi uliyofutwa ulikuwa halali."Hatutatambua matokeo ya uchaguzi huu haram, na tutaendelea kupigiania demokrasia visiwani Zanzibar," alisema Mazrui katika mahojiano na DW.
Takwimu za tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC, zinaonyesha kuwa wapigakura 503,860 walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo kulikuwa na jumla ya vituo vya kupigia kura 1,580 na kila kituo kina wastani wa wapigakura 350.
CCM yaridhishwa na mchakato mzima
Rais wa sasa Ali Mohammed Shein anatafuta muhula wa pili kupitia chama tawala - chama cha Mapinduzi CCM. Shein aligombea katika uchaguzi wa Oktoba dhidi ya mpinzani wake mkuu Seif Sharif Hamad ambaye pia alikuwa makamu wa kwanza wa rais kulingana na katiba ya Zanzibar.
Akizungumza na DW baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura, naibu katibu mkuu wa CCM kwa upande wa Zanzibar Vaui Ali Vuai alisema zoezi hilo la uchaguzi lilikwenda kwa amani na kuelezea matumaini kuwa wananchi watadumisha utulivu hadi kukamilika kabisaa za zoezi zima la uchaguzi.
"Kwa ujumla zoezi zima limekwenda kwa amani kwa maana ya amani, usalama na utulivu katika vituo vya kupigia kura na kila mwenye haki ya kupiga ya kupiga kura alitekeleza haki yake," alisema Vuai katika mahojiano na DW.
Maalim Seif alidai ushindi kabla ya kutangazwa kwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa Oktoba - na hii ikawa moja ya hoja zilizotolewa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzu Jecha Salum Jecha, wakati akifuta matokeo ya awali. Hamad amekuwa akigombea urais wa Zanzibar tangu uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.
Licha ya kuwepo na hali ya taharuki kuelekea uchaguzi huo, hali ilikuwa tofuati hapo jana ambapo maeneo mengi yalionekana kuwa na amani na pia vikosi vya usalama havikujitokeza barabarani kama ilivyozoeleka.
CUF na miaka 15 ya majaribio
Chama cha CUF kimekuwa kikijaribu kwa miaka kadhaa kuiondoa CCM madarani visiwani humo, kikipoteza kwa tofauti ndogo sana katika uchaguzi wa mwaka 2010. Zoezi la kuhesabu kura lilianza baada ya kufungwa kwa vituo majira ya saa jioni, na matokeo kamili yantarajiwa katika muda usiyozidi siku tatu.
Zanzibar ni sehemu ya Tanzania yenye mamlaka yake ya ndani, ikiwa na rais wake, lakini wakaazi wengi visiwani hapo wanalalamika kwamba serikali ya muungano ndiyo inaamuwa sera, hasa kwenye masuala ya kiuchumi.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/APE, DW
Mhariri: Sudi Mnette