1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Djibouti yavutia majeshi ya kimataifa

9 Agosti 2016

Djibouti imekuwa kivutio cha majeshi ya mataifa mbalimbali duniani kutokana na mahali ilipo. Taifa hilo katika pembe ya Afrika lenye wakazi kiasi ya 800,000 limejaa kambi za majeshi ya mataifa yenye nguvu duniani.

https://p.dw.com/p/1JeTx
Dschibuti im Hafen Japanisches Militär
Jeshi la Japan katika Bandari ya DjiboutiPicha: picture-alliance/dpa

Meli ya kivita ya Ufaransa hufanya safari ya baharini kati ya Afrika na Uarabuni katika luteka za pamoja za kijeshi na Marekani, hali inayodhihirisha jukumu muhimu la kimkakati la Djibouti kwa majeshi ya mataifa makubwa. Katika pwani ya taifa hilo la pembe ya Afrika wanajeshi wapatao 500 wa Ufaransa hutembea pamoja na wanajeshi 50 wa Marekani karibu na mji wa Arta, wakiwa wamevalia sare za kijeshi.

Mazoezi hayo ya kijeshi yanayonuiwa kuwasaidia washirika hao wawili, pia yanatoa taswira ya mvuto wa kimataifa unaozidi kuongezeka kwa nchi hiyo iliyokuwa koloni la Ufaransa, inayopakana na Somalia na ikiwa sio mbali sana na Yemen.

Ikiwa na wakazi wapatao 800,000, Djibouti sasa imejaa kambi za kijeshi za mataifa kadhaa yenye nguvu duniani. Bandari yake hutumiwa kuilinda bahari ya Shamu na mfereji wa Suez katika njia ya baharini yenye shughuli nyingi kabisa duniani.

"Hii bila shaka ndio sababu kwa nini pamoja na wanajeshi wa Ufaransa, leo kuna vikosi vingi vya kimataifa vinavyotaka kuwepo Djibouti," amesema Jenerali Philippe Montocchio, Kamanda wa vikosi vya Ufaransa nchini humo. "Kuna Wamarekani, Wajapani, Wataliani, na sasa Wachina, na bila shaka katika siku zijazo, Wasaudi," akaongeza kusema kamanda huyo.

Ilibainika miezi minne iliyopita kwamba China ilikuwa imesaini makubaliano na Djibouti ya kujenga kambi ya jeshi lake la majini kufikia mwisho wa mwaka ujao 2017. China itawaweka wanajeshi wake hadi 10,000 katika kambi hiyo itakayotumiwa kuyalinda masilahi ya China yanayoendelea kuongezeka katika eneo hilo. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa China kuwa na tume ya kudumu ya kijeshi nje ya nchi.

Mapambano dhidi ya ugaidi na uharamia

Camp Lemonnier, kambi pekee ya kudumu ya jeshi la Marekani barani Afrika inapatikana Djibouti. Inatumiwa kwa mapambano ya siri dhidi ya ugaidi na harakati nyingine nchini Yemen, pamoja na vita vya Marekani dhidi ya kundi la al Shabaab nchini Somalia na Al-Qaeda katika rasi ya Uarabuni, AQAP. Marekani inasema inailipa Djibouti kiasi dola milioni 60 kila mwaka kwa ajili ya kambi hiyo.

Chinesisches Kriegsgerät Anti-Piraten Einsatz Somalia
Meli ya China ikipiga doria katika Pwani ya SomaliaPicha: picture alliance/dpa/Z. Kun Qd

Majeshi ya majini ya nchi za Ulaya na mataifa mengine huitumia bandari ya Djibouti kama eneo la kuratibu mapambano dhidi ya uharamia kutoka kwa maharamia wa taifa jirani la Somalia. Eneo la bahari ni muhimu lakini pia wakati mwingine huwa hatari. Huku majeshi ya kimataifa yakiwa baharini, mashambulizi ya maharamia ya kisomali yamepungua. Kwa mujibu wa jeshi la majini la Ulaya, mashambulizi 176 yalirekodiwa mwaka 2011 na hakuna shambulizi lolote lililotokea mwaka 2015.

Na kilometa 30 kutoka ghuba ya Aden inapatikana nchi ya Yemen iliyoharibiwa na vita vya wenyewe ambavyo vimeshuhudia waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, wakipambana na serikali inayotambuliwa kimataifa inayosaidiwa na mashambulizi ya kutokea angani ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

Makundi ya kiislamu yakiwemo kitengo cha al Qaeda nchini Yemen, na wapiganaji wa dola la kiislamu, wamejiunga na vita hivyo vya kung'ang'ania madaraka nchini humo. "Djibouti inapatikana katika kitovu cha vuguvugu hili la wapiganaji wa jihadi katika pembe ya Afrika na eneo la kusini la Mashariki ya Kati," amesema kamanda wa vikosi vya Ufaransa nchini Djibouti, Jenerali Philippe Montocchio.

China, mbali na kambi ya jeshi la majini, inafadhili miradi mikubwa ya miundombinu nchini Djibouti, ikiwemo viunganishi vya usafiri kwa masoko muhimu katika nchi jirani ambayo haipakani na bahari ya Ethiopia.

"Kila mtu alishangaa: kwa nini China? Kwa Djibouti hakuna suali," alisema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Djibouti, Mahamoud Ali Youssouf. "Uwepo wa China, baharini au kijeshi, ni sehemu ya mantiki ya mataifa mengine yenye uwezo wa kuchangia juhudi za kudumisha amani na usalama katika eneo ambalo linakabiliwa na migogoro," akaongeza kusema waziri huyo.

Lakini kujiingiza kwa China katika kile kinaoelezwa kuwa "Mchezo Mkubwa" ni kamari hatari kwa Djibouti - huenda kukavuruga mahusinao na washirika wa tangu jadi, hususan Marekani.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe

Mhariri: Daniel Gakuba