1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Djibouti yaiomba UN kumaliza mzozo na Eritrea

19 Julai 2018

Djibouti imemuomba katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guerres kusaidia mpango wa kusaka suluhu ya amani katika mzozo unaofukuta wa mpaka na Eritrea, baada ya ule kati yake na Ethiopia uliodumu kwa miaka 20.

https://p.dw.com/p/31lqr
23.02.2013 DW online Karte Djibouti eng

Balozi wa Djibouti katika Umoja wa Mataifa Mohamed Siad Doualeh, alimuomba Guterres kupitia barua iliyosambazwa Jumatano hii, kushirikiana na baraza la usalama la Umoja huo, ya kuzikutanisha pamoja Eritrea na Ethiopia kwa lengo la kuwezesha makubaliano baina yao kwa kutumia mbinu za amani zinazokubalika na pande zote.

Ombi hilo la Djibouti kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, linakuja baada ya kurejeshwa kwa mahusiano mazuri ya kidiplomasia katika taifa hilo la Afrika, katika mchakato ulioanza mwezi uliopita, wakati waziri mkuu mpya wa Ethiopia alipokubaliana kikamilifu na makataba wa amani uliohitimisha vita vya kugombania mpaka vya kati ya mwaka 1998 hadi 2000 na Eritrea, vilivyosababisha vifo vya maelfu ya raia.

Doualeh alikumbushia vikwazo vilivyowekwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa vilivyowekwa nchini Eritrea mwaka 2009, kufuatia uchokozi wake dhidi ya Dhibouti pamoja na hatua yake ya kupinga kuondoa wanajeshi wake katika eneo linalozozaniwa, lakini pia kukataa juhudi zote zilizolenga kusaka suluhu baina ya pande hizo mbili.

Schweiz - UN-Generalsekretär in Genf
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ndiye anayeombwa kuingilia kati mzozo huo wa Djibouti na EritreaPicha: picture-alliance/Keystone/C. Zingaro

Kati ya mwaka 2010 na 2017, Qatar ilijaribu kusuluhisha mzozo huo, lakini juhudi zake zilishindwa, na hatimaye ikaondoa wanajeshi wake 450 wa kulinda amani waliokuwa kwenye eneo la mpakani. Djibout iliwatuhumu wanajeshi wa Eritrea kwa kulichukua eneo la mlima wa Dumeira muda mfupi baada ya walinda amani kuondoka Juni 13, 2017, hatua iliyopelekea kuwasilisha malalamiko rasmi katika Umoja wa Afrika. 

Kulingana na balozi Doualeh, majeshi ya Eritrea yameendelea kuchukua maeneo ya Djibouti na wafungwa wa kivita wameendelea kupuuzwa. Amesema, Eritrea imeendelea kutoa vitisho vya matumizi ya nguvu, na kwa mara nyingine kuna wasiwasi mkubwa wa kuzuka kwa makabiliano. 

Ameonya kwamba bila ya juhudi zozote za kumaliza mzozo wa mpaka, kundi la waangalizi la Umoja wa Mataifa limesema, hali katika eneo hilo itaendelea kukabiliwa na hatari dhidi ya uchokozi kutoka pande zote mbili, ambayo huenda ikasababisha kusambaa kwa haraka kwa mapigano. Amesema, kutokana na hali hiyo ni lazima kutafutwa kwa njia mpya za dharura za kupata suluhisho.

Balozi huyo pia amesema Djibouti imesifu maamuzi ya hivi karibuni ya katibu mkuu Guterres ya kuwasilisha mzozo wa muda mrefu wa mpaka kati ya Venezuela na Guyana kwenye mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ. Lakini pia, aligusia Eritrea ambayo imefanikiwa kusuluhisha mzozo wa mpaka wa bahari na Yemen, pamoja na kisiwa cha bahari ya Shamu, kupitia usuluhishi wa kimataifa.  

Amesema, Djibouti itazingatia kwa nia njema mapendekezo yoyote ambayo katibu mkuu Guterres ama baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linaweza kuyatoa kwa kuzingatia namna muafaka ya kuumaliza mzozo kwa amani.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE

Mhariri: Josephat Charo