Di Matteo aanza majukumu kama kocha wa Schalke
17 Oktoba 2014Licha ya kufuzu katika Champions League, Schalke kwa sasa wako katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi na wamempa majukumu nyota wa zamani wa Italia di Matteo kuchukua nafasi ya Jens Keller aliyetimuliwa. Di Matteo alifanya mazoezi ya fargaha na Schalke na anataka wawe na mwanzo mzuri na Hertha Berlin ambao wako katika nafasi ya 12. Anasema "Bila shaka utakuwa mchuano mgumu. Walimsajili mchezaji mzuri sana, Salomon Kalou, ambaye anaweza kutatiza sana safu ya ulinzi lakini lazima tuwe makini na kuhakikisha kuwa tunawasumbua sana. Utakuwa mpambano ambao subira itahitajika lakini wachezaji wamejawa na hamasa na tungependa kushinda mchezo huo katika njia nzuri".
Mwenzake wa Hertha Berlin Jos Luhukay anasema utakuwa ni mpambano mgumu hasa ikizingatiwa kuwa Schalke wamepata mkufunzi mpya ambaye analenga kuwa na mwanzo mzuri."Tunaiheshimu timu ya Schalke. Tunafahamu kuwa wana ubora wa hali y ajuu na ni hatari sana katika mashambulizi wakiongozwa na Klaas-Jan Huntelaar ambaye ni hatari sana katika lango na atakuwa tishio kubwa. Yeye huifungia Schalke magoli muhimu"
Kileleni mwa msimamo wa ligi, Bayern Munich wanalenga kupanua uongozi wao kwa pointi nne wakati wakiwaalika Werder Bremen uwanjani Allianz Arena. Bremen wamepata vichapo mikononi mwa Bayern katika mechi zao tatu za mwisho. Bayern walipata habari mbaya katikati ya wiki baada ya kubainika kuwa kiungo wa Uhispania Thiago Alcantara anastahili kufanyiwa upasuaji mpya baada ya kuumia tena goli lake.
Na hata nyota kama vile Bastian Schweinsteiger, Franck Ribery na Javi Martinez wakiwa kwenye orodha ya muda mrefu ya majeruhi, kocha wa Bayern Pep Guardiola bado ana kikosi imara.
Kwingineko, Borussia Dortmund wanahitaki kuifufua kampeni yao ya Bundesliga wakati watakapochuana na FC Cologne ugenini huku kocha Jurgen Klopp akidai mwanzo mpya kutoka kwa vijana wake.
Viungo wa Ujerumani Marco Reus na Ilkay Gundogan pamoja na Henrikh Mkhitaryan wa Arminia wanajizatiti kurejea kutoka mkekani. Mechi nyingine za leo ni Mainz 05 v Augsburg, Hanover 96 v Borussia Moenchengladbach, Freiburg v VfL Wolfsburg, VfB Stuttgart v Bayer Leverkusen. Hapo kesho, Hamburg v Hoffenheim, Paderborn v Eintracht Frankfurt
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu