Dhoruba Ana yasababisha vifo vya watu 11 nchini Msumbiji
26 Januari 2022Siku ya Jumanne, taasisi ya kitaifa ya usimamizi na uthibiti wa athari za majanga, ilisema kuwa watu wanane walifariki dunia na wengine 54 kujeruhiwa huku wengine 895 wakihamishwa katika maeneo salama masaa 24 mapema. Taasisi ya INGD imesema kuwa zaidi ya watu 20,000 nchini Msumbiji wameathirika kutokana na dhoruba hiyo, na zaidi ya nyumba 3,000 zimeharibiwa kwa sehemu huku zaidi ya nyumba 600 zikiharibiwa kabisa pamoja na vituo kadhaa vya afya na madarasa na kuongeza kuwa ndege zisizo na rubani na boti zimepelekwa katika juhudi za kutoa msaada.
Katika nchi jirani ya Malawi, ambapo dhoruba hiyo ilisababisha kukatika kwa nguvu za umeme kutokana na mafuriko yalioharibu mitambo ya umeme, kamishna wa wilaya ya Chikwawa alithibitisha vifo vingine vitatu, baada ya idara ya maafa Jumanne kuripoti kifo kimoja huko Mulanje. Wataalamu wanasema dhoruba zimekuwa na nguvu zaidi kwasababu maji yamepata joto kutokana na mabadiliko ya tabianchi wakati kupanda kwa viwango vya bahari kukisababisha maeneo ya chini kukabiliwa na hatari.
Bidhaa zinazohitajika kwa dharura
Naemi Heita, kaimu mkuu wa ujumbe wa shirikisho la kimataifa la mashariki ya msalaba mwekundu na lile la Red Crescent, ameliambia shirika la habari la reuters kwamba maji safi ya kunywa, vyandarua vya kuzuia mbu na barakoa ni baadhi ya vitu vinavyohitajika kwa haraka kuzuia milipuko ya magonjwa. Heita ameongeza kuwa mbali ya hatua za dharura za msaada, wanahitaji kuhakikisha wanazisaidia familia kujenga upya maisha yao kwasababu mashamba yamejaa maji na nyumba kuharibika.
Msumbiji na nchi nyingine za kusini mwa Afrika zimekuwa zikikabiliwa na mafuriko ya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni ambayo yameharibu miundombinu na kusababisha idadi kubwa ya watu kuyahama makazi yao. Zaidi ya watu 100 tayari wamefariki katika mafuriko nchini Afrika Kusini, Lesotho na Madagascar, ambako uharibifu wa mali umekadiriwa kuwa wa mamilioni ya pesa.
Hivi sasa ni msimu wa kimbunga cha kiangazi katika eneo la kusini mwa Afrika, ambacho kinaweza kusababisha dhoruba kali na mvua hadi kufikia mwezi Machi ama Aprili.