Deutsche Welle yapata Mkurugenzi Mkuu mpya
18 Machi 2013Limbourg mwenye umri wa miaka 52 alichaguliwa mjini Berlin na Baraza hilo la Utangazaji wa Radio kwa kura 14 .Kura moja ilikuwa ya kupinga na wajumbe wawili hawakupiga kura.
Mpaka sasa mwandishi huyo wa habari alikuwa mkurugenzi wa habari kwenye Shirika la Televisheni la Ujerumani la ProSiebnSat1. Kutokana na pendekezo la tume ya wakurugenzi, Limbourg alipita katika duru ya kwanza ya kupiga kura.
Limbourg anazo sifa zote atakazokuja nazo DW na hivyo kuweza kuiimarisha DW kama chombo cha kisasa cha habari cha matangazo ya nchi za nje. Pia anakuja DW na uwezo wa kuiimaisha dhima ya DW katika medani ya kimataifa.
Limbourg ni mwandishi habari mwenye sifa siyo tu kuwa na tajiriba ya kimataifa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingi na mwenye umahiri katika usimamizi wa vyombo vya habari, amesema Mwenyekiti wa Baraza la Utangazaji la Radio ,Valentin Schmidt.
Mkurugenzi Mkuu mpya kuendeleza zaidi uanuai wa lugha
Limbourg amewashukuru wajumbe wa Baraza kwa kumpa imani yao. Amesema katika miaka inayokuja, atatumia uwezo wake katika kuikabili changamoto ya kulitangaza jina zuri la Ujerumani duniani, kwani matangazo ya DW yamekuwa sehemu ya tajiriba ya maisha yake tokea siku za ujana wake alipokuwa katika nchi za nje.
Limbourg ameahidi kushirikiana na wafanyakazi wote kwa lengo la kuuendeleza wajihi wa kiuandishi wa DW, uanuai wa lugha na kuimarisha nyanja zote za mawasiliano katika DW.
Mkurugenzi huyo mteule amesema pia anakusudia kuimarisha ushirikiano baina ya DW na mashirika ya televisheni za serikali za ARD na ZDF.
Kitaaluma mkurugenzi huyu mpya ni msomi wa mambo ya sheria mjini Bonn baada ya kulitumikia jeshi. Kuanzia mwaka wa 1988 hadi 1989, alifanya kazi ya hiari katika shirika la televisheni la Ujerumani (DFA) mijini Bonn na London. Baada ya kuwa mwandishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani, akiwa na makao katika mji wa Leipzig, Limbourg alikuwa mwandishi masuala ya bara la Ulaya wa mashirika ya DFA na SAT1 kuanzia mwaka wa 1990.Pia aliripoti juu ya NATO, akiwa na kituo chake katika mji wa Brussels, Ubelgiji.
Mnamo mwaka wa 1999 Limbourg alikabidhiwa uongozi wa ofisi ya shirika la ProSieben.Mnamo mwaka huo huo aliteuliwa kuwa mhariri mkuu mwenza wa shirika la N 24 na aliteuliwa kuwa mkuu wa masuala ya kisiasa wa shirika la ProSieben.Alikabidhiwa wajibu huo pia kwa SAT1 .
Kwa sasa, Limbourg ni mwenyekiti wa jopo la vyombo vya la Bunge la Ujerumani, na pia mjumbe wa jopo la kitengo kinachosimamia vipaji vya waandishi vijana kwenye shirika la Axel Springer na mshauri wa mambo ya habari kwenye kamati ya Baraza la Maaskofu la Ujerumani.
Limbourg aliyezaliwa mjini Bonn, alikulia katika miji ya Rome, Paris, Athens na Brussels. Ana mke na watoto watatu.Sasa anachukuwa nafasi ya Erik Betterman mwenye umri wa miaka 68 na anayemaliza rasmi utumishi wake kwenye DW ifikapo mwezi Septemba.
Mwandishi: HA Kommunikation/Desk
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Khelef