1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deutsche Welle yaadhimisha miaka 65 tangu kuasisiwa

Josephat Charo
5 Juni 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema (05.06.2018) Deutsche Welle ni chombo kinachosimamia uandishi habari makini wa kuaminika na usioegemea upande wowote.

https://p.dw.com/p/2yzV9
Bundeskanzlerin Angela Merkel und DW-Intendant Peter Limbourg beim Festakt 65 Jahre DW
Picha: DW/J. Roehl

Akiwa na shauku kubwa Kossivi Tiassou, amemuelezea kansela Merkel kwamba mradi wa utengenezaji wa kipindi cha televisheni wa "Eco@africa" chini ya ushirikiano baina ya Ulaya na Afrika umepata mafanikio makubwa. Kupitia mada hii kipindi hicho cha Mazingira cha Deutsche Welle kimefaulu kuwafikia mamilioni ya watazamaji katika sehemu nyingi za bara la Afrika.

"Unatokea wapi?" aliuliza kansela Merkel. "Togo," akajibu Tiassou. Kansela akadokeza hajawahi kufanya ziara nchini humo lakini angependelea siku moja kwenda kutembea. Na alifurahia sana kwamba kipindi hiki cha mazingira kinafuatiliwa na kupendwa sana barani Afrika.

Dakika chache baadaye Merkel alisimama mbele ya kipaza sauti na kuipongeza kazi inayofanywa na Deutsche Welle na kuzungumzia tena mradi wa Eco@africa". Aliona "ni jambo maridhwawa kabisa kwamba Deutsche Welle inaandaa kipindi cha mazingira Afrika kinachotoa taswira ya masuala ya bara hilo," alipongeza. Hatimaye kansela Merkel akawa pia waziri wa mazingira.

Katika hotuba ya dakika 15 kansela Merkel alisisitiza umuhimu na maana ya Deutsche Welle tangu ilipoanzishwa 1953 mpaka hivi sasa, wakati wa mizozo ya miaka ya 1950 na 1960 kama ilivyo katika migogoro ya sasa. "Deutsche Welle ni hadhithi ya mafanikio na inahitajika sana kuliko wakati mwingine wowote ule," alisema Merkel. Kituo hiki cha matangazo kimekuwa cha kisasa zaidi, cha kuvutia zaidi na cha kimataifa zaidi kila mwaka. Deutsche Welle inasimamia uandishi habari wa kuaminika, wa kutegemewa na usiopendelea upande wowote."

Bundeskanzlerin Angela Merkel, DW-Intendant Peter Limbourg und Staatsministerin Prof. Monika Grütters, Beauftragte der Bundesregierung für Kultur und Medien, beim Festakt 65 Jahre DW
Kutoka kushoto: Kansela Merkel, Peter Limbourg, Mkurugenzi wa DW na Prof Monika Grütters, waziri wa utamaduni na michezo wa UjerumaniPicha: DW/J. Roehl

Sauti huru

Wakati wa hotuba yake iliyojaa hisia, Merkel alizungumzia ukweli halisi wa kisiasa. Katika ulimwengu ambao umeunganishwa, mawasiliano ya kimataifa yanaendelea kuwa muhimu zaidi kila uchao. Kwa kuwa sio sadfa kwamba baadhi ya nchi zinavitanua vituo vyao vya kimataifa vya matangazo, tukitazama Urusi au China. "Na kama ilivyo kuhusiana na masuala ya biashara na China, tunataka pia mabadilishano kwa vyombo vya habari vya kimataifa. Hilo ndilo tunalolitaka kwa Deutsche Welle pia."

Kansela Merkel alisema kwa ujumla hadi kufikia leo Deutsche Welle imekuwa sauti ya uhuru na haijaathiriwa, bali imepigwa vita na kuzuiwa.

Mwanzoni mwa shughuli ya maadhimisho ya miaka 65 ya Deutsche Welle, muongozaji matangazo Jaafar Abdul-Karin aligusia nembo ya DW mbele ya wabunge kadhaa: lugha 30, nchi 60, akisafiri katika sehemu mbali mbali za ulimwengu. Halafu alisema "Nilikuwa mji wa Mosul wiki tatu zilizopita.."

Kama ushahidi picha za kipindi chake cha mjadala kwa lugha ya kiarabu "Shabab Talk" baadaye zilioneshwa: Abdul Karim alikaa kwenye viti vya plastiki na washiriki walioalikwa kwa mazungumzo pamoja na wasikilizaji wakiwa kati ya magofu marefu kaskazini mwa Iraq, mfano ambao unadhihirisha kwamba DW hufuatilia masuala tete yanayogusa hisia za watu.

Karsai, Mogherini, Wenders, Solschenizyna

Wengi walikubaliana na matamshi ya kansela Merkel. Katika jukwaa, mwenyekiti wa kamati ya bunge inayohusika na masuala ya utamaduni, Katrin Budde, wa chama cha Social Democratic SPD na waziri wa dola Monika Grütters wa chama cha Christian Democratic Union, CDU. Grütters alisema, "DW inasimamia uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa  habari, utafiti wa kina na uandishi mzuri wa habari, uhuru wa vyombo vya habari, utangazaji wa umma. Kwa hayo ninajivunia sana." Na aliwataka wasikilizaji wapakaue app ya DW ili waweze kupata taswira nzuri zaidi ya matangazo na jinsi shirika hili linavyojishughulisha kwa ajili ya binadamu katika maeneo ya mizozo.

Festakt 65 Jahre DW mit Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela Merkel akiwa mgeni wa heshima katika jumba la Paul-Löbe mjini Berlin kulikofanyika maadhimishoPicha: DW/J. Roehl

Kupitia video walizungumza mawaziri wa shirikisho kutoka vyama vya CDU na SPD, spika wa bunge la Ujerumani, Wolfgang Schäuble, wanasiasa wa wa chama cha Kijani, chama cha Die Linke na FDP, wanasiasa wa kimataifa kama vile rais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, mkuu wa sera za Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, na rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karsai. Walikuwepo pia watu mashuhuri katika utamadunini Nike Wagner, Wim Wenders na Natlja Solschenizyna, mjane wa mwandishi wa Urusi, Alexander Solzhenitsyn. Na mchezaji wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani, Jerome Boateng, pia alikuwapo.

Mwandishi: Strack, Christoph

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri: Grace Kabogo