1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Desertec - Joto la jua kuzalisha Nishati

14 Julai 2009

Jumatatu,mradi mkubwa kabisa wa nishati endelevu ulizinduliwa Munich,Ujerumani.Mradi huo Desertec,unatazamia kuzalisha nishati kwa kutumia miale ya jua jangwani Afrika na kuipeleka nishati hiyo safi katika nchi za Ulaya.

https://p.dw.com/p/Ioxj

Lakini mradi huo utazinufaisha vipi nchi za Kiafrika? Je, baada ya kuporwa raslimali, sasa nchi hizo zitaporwa jua lake pia? Au, huo ni mradi utakaosaidia kutoa nafasi za ajira na kukidhi mahitaji ya nishati? Kila mwaka nchini Misri, jua hupiga kwa saa 3,000 na wakati mwengine, vipimo vya joto hupindukia sentigredi 40 Celsius. Joto hilo, linaweza kutumiwa kuzalisha nishati. Eneo lenye joto kali ni kubwa vya kutosha,kwani asilimia 96 ya nchi hiyo ni jangwa. Hata nchini Libya au Sudan hali si tofauti.

Badala ya kuchimbua raslimali zake za mafuta na gesi ili kuzalisha nishati inayolipiwa ruzuku nyumbani, nchi hizo zingeweza kutumia jua kupata nishati inayohitajiwa na mafuta yake yakauzwa nje au nchi hizo zingeweza pia kusafirisha nishati safi inayopatikana bila ya kuchafua mazingira.Vile vile kuna faida za kiuchumi, nishati inapozalishwa kwa kutumia joto la jua. Hapo, mashine huendeshwa kwa maji yaliyofanywa kuwa mvuke, sawa na mitambo inayotumia gesi au makaa.

Lakini, kuna tofauti moja, hakuna moto unaotumiwa kupata mvuke huo, bali jua moja kwa moja, hutoa joto linalohitajiwa. Na utaratibu huo wala si mgumu. Mtu anaweza kusema kuwa ni mradi unatoa nafasi nzuri kwa nchi za Kiafrika. Kwa mfano, vioo vinavyohitajiwa kudaka miyale ya jua na mabomba yanayokusanya mvuke, yangeweza kutengenzwa katika nchi zenye mitambo hiyo ya nishati. Na ikiwa makampuni ya Ulaya yatapeleka ujuzi wake na mashine zinazohitajiwa, basi baada ya muda mitambo hiyo yenye teknolojia ya kisasa itaweza kutengenezwa kule kule ambako joto la jua hutumiwa kuzalisha nishati safi.Hivyo, nchi za Kiafrika zitaweza kunufaika kwa njia mbali mbali; zitapata nafasi mpya za ajira, zitakidhi mahitaji yake ya nishati, hasa katika nchi za Kiarabu ambako mahitaji ya nishati, yanatazamiwa kuongezeka sana katika karne ijayo; na pia nishati ziada inaweza kuuzwa katika nchi za Ulaya kwa faida.

Lakini hiyo humaanisha kuwa makampuni ya Kijerumani yatakayosimamia gharama za mradi wa Desertec hazitopata faida kubwa sana. Kwani makampuni hayo hayatopeleka mashine za mitambo hiyo, bali ujuzi wa kuijenga mitambo hiyo. Lakini yatabakia kama wawekezaji na yatahusika pia na usafirishaji wa nishati barani Ulaya. Lakini kilicho muhimu zaidi ni kuwa katika nchi za Afrika ya Magharibi, nishati mbadala ni nishati inayozalishwa na mitambo ya nyuklia. Kwa mfano, Misri inajadiliana na Russia kusaidiwa kujenga mtambo wa kuzalisha nishati ya nyuklia. Libya imeshakubaliwa na Ufaransa. Hiyo pekee ni sababu ya kutosha kueneza utaratibu wa kuzalisha nishati kwa kutumia joto la jua. Kwanza, utaratibu huo ni salama na hauchafui mazingira. Isitoshe, Ulaya na Afrika zitanufaika kupiga vita mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwandishi: Saoub, Esther/ZR

Mhariri: Miraji Othman