1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dereva wa Osama Bin Laden mahamakani Guantanamo

Othman, Miraji6 Agosti 2008

Dereva wa Osama Bin Laden mahakamani Guantanamo

https://p.dw.com/p/ErNO
Mlinzi wa jeshi la Kimarekani katika gereza la GuantanamoPicha: AP

Wazee wa mahakama ya kijeshi ya Kimarekani huko Guantanamo leo wataendelea na mashauriano yao katika kesi inayomkabili dereva wa Osama Bin Laden, licha ya kwamba mawakili wa mshtakiwa huyo na wanaharakati wa haki za binadamu wameuelezea mfumo wa mahakama hiyo kuwa usiokuwa wa haki. Pia mjini New York, hakimu jana aliamuru mwanamke wa Kipakistani anayeshukiwa kuwa na maingiliano na viongozi wa ngazi za juu wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaida abakishwe kizuizini hadi wiki ijayo, akishtakiwa kujaribu kuwauwa wanajeshi wa Kimarekani nchini Afghanistan.

Mawakili wa dereva wa zamani wa Osama Ben Laden, Salim Hamdan, walisema kesi kamili ya mteja wao, inayosikilizwa katika mahakama maalum ya kijeshi ilioundwa na Rais George Bush, imedhihirisha kwamba mfumo huo umesukwa kuupendelea upande wa mashtaka, ukiruhusu ushahidi na maelezo ya tetesi; tena ushahidi umepatikana kwa njia ya kuwalazimisha watu.

Maafisa sita wa jeshi, kama wazee wa mahakama, wanajitayarisha katika siku ya tatu ya kesi hiyo ambapo inatakiwa ijulikane kama Salim Hamdan alifanya njama na kuusaidia mtandao wa kigaidi wa al-Qaida. Mawakili wa mshtakiwa walisema kesi hiyo inakosa baadhi ya haki za kimsingi ambazo zinatakiwa ziweko katika mahakama yeyote ya Kimarekani. Alipoulizwa kama ana imani na wazee wa mahakama wanaopima ushahidi dhidi ya mteja wake, mmoja wa mawakili wa Salim Hamdan alisema tatizo haliko katika wazee wa mahakama, lakini liko katika mfumo wa kesi yenyewe.

Waendeshaji mashtaka na maafisa wa jeshi la Marekani walisema mahakama hiyo inawapa washukiwa haki, wakihoji kwamba magaidi wanaotuhumiwa hawawezi kuangaliwa kama wanajeshi wa kawaida wanaowajibika kwa jeshi la nchi.

Salim Hamdan, raia wa Yemen, ambaye ameshatumikia zaidi ya miaka sita katika gereza la Guantanamo, alionekana ana wasiwasi pale alipokuweko mahakamani. Waendeshaji mashtaka walidai kwamba Salim Hamdan alikuwa sehemu ya duru ya ndani ya Ben Laden na alisaidia kusafirisha silaha. Lakini mawakili wake walisema yeye ni samaki mdogo ambaye hahusiani na njama za mtandao wa al-Qaida. Wanaharakati wa kupigania haki za binadamu wamelalamika kwamba mitindo ya ajabu ya kuhoji katika kupata ushahidi iliruhusiwa, na kwamba taarifa zilizotolewa huko Guantanamo ziliruhusiwa kama ushahidi, licha ya kwamba Salim Hamdan alinyimwa sana usingizi, alitishiwa kuingiliwa kimapenzi na kufanyiwa uonevu mwengine. Wazee wa mahakama wana kazi ngumu ya kuamua kitendo gani kinaweza kutiwa katika kundi la uhalifu wa kivita, japokuwa hakimu amewataka waamuwe kama kusafirisha maroketi ya kushambulia kutoka ardhini hadi angani dhidi ya majeshi ya Kimarekani ni jambo linaloangukia katika uhalifu wakivita.

Wakati huo huo, jana mahakama ya New York iliamuru mwanamke wa Kipakistani anayeshukiwa kuwa na maingiliano ya ngazi ya juu na mtandao wa al-Qaida awekwe kizuizini hadi wiki ijayo, akishtakiwa kujaribu kuwauwa wanajeshi wa Kimarekani nchini Afghanistan. Aafia Siddqui, mwenye umri wa miaka 36, atafikishwa tena mahakamani ili iamuliwe kama aachiliwe huru kwa dhamana. Hajakiri kama ana hatia, lakini mawakili wake walihoji kwamba mama huyo, mwenye watoto watatu, alikuwa hana hatia. Walikanusha kwamba Aafia Siddiqui alikuwa na maingiliano na mtandao wa al-Qaida. Mshtakiwa huyo, aliyesomea sayansi ya tiba huko Massachusetts alipigwa risasi na kujeruhiuwa wakati inadaiwa alipokuwa anajaribu kuwafyetulia risasi wanajeshi wa Kimarekani waliokwenda kumhoji katika mkoa wa Ghazni huko Afghanistan. Mwaka 2004 shirika la upelelezi la Marekani, FBI, lilimtaja bibi huyo kuwa ni hatari kwa Marekani. Yeye aliolewa na bin ami wa Khalid Sheikh Mohammed, ambaye alisaidia kupanga mashamuulio ya Septemba 11 huko New York. Mume wake alikamatwa mwaka 2003 na hivi sasa anazuiliwa katika gereza la Guantanamo.