Denmark yaridhia kujiunga na sera ya ulinzi barani Ulaya
2 Juni 2022Matokeo ya mwisho ya kura hiyo ya maoni yameonesha karibu asilimia 70 ya raia waliojitokeza kupiga kura wameunga mkono hatua ya nchi hiyo kujiunga na sera ya pamoja ya ulinzi ya Umoja wa Ulaya.
Ni asilimia 33.1 tu wapigakura ndiyo wamepinga pendekezo hilo. Matokeo hayo ni mabadiliko makubwa kuwahi kufanywa na nchi hiyo ambayo kwa muda mrefu imejitenga na ushirikiano wa kijeshi wa mataifa ya Ulaya.
Ushindi wa kura hiyo ya maoni unamaanisha Denmark itaanza kushiriki kwenye mipango yote ya pamoja ya ulinzi na usalama ndani ya Umoja wa Ulaya katika siku zijazo.
Miongoni mwa mengine ni kuchangia wanajeshi katika ujumbe wa kulinda amani wa Umoja huo unaotumwa kwenye mataifa ya kigeni.
Kabla ya kura hiyo Denmark ndiyo ilikuwa nchi pekee ya Umoja wa Ulaya isiyoshiriki kwenye shughuli za ulinzi na usalama wa kanda hiyo baada ya kukataa kuidhinisha sera ya pamoja iliyopitishwa mwaka 1993.
Viongozi wayakaribisha matokeo ya kura ya maoni kwa bashasha
Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen amesema matokeo hayo yametuma ujumbe kwamba nchi hiyo ni mshirika wa kutumainiwa katika kulinda uthabiti wa bara la Ulaya.
"Usiku huu Denmark imetuma ishara muhimu sana. Kwa washirika wetu wa Ulaya na Jumuiya ya NATO, na kwa Putin. Tunadhihirisha kwamba wakati Putin akiivamia nchi huru na kutishia utulivu barani Ulaya, sisi tunajiunga pamoja" amesema bibi Frederiksen.
Matamshi sawa na hayo yametolewa pia na kiongozi wa upinzani nchini Denmark Jakob Elleman Jensen aliyesema ushindi wa kura hiyo ni salamu kwa wale wasioitakia mema nchi hiyo na wote wanaotaka vita barani Ulaya.
Matokeo ya kura hiyo yamekaribishwa kwa bashasha na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya. Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa huo Ursula von der Leyen ameandika kupitia ukurasa wa Twitter kuwa uamuzi huo wa Denmark ni "ujumbe mzito wa utayari katika ulinzi wa pamoja".
Naye kiongozi wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel kwa upande wake ameisifu nchi hiyo na kuyataja matokeo ya kura hiyo ya maoni kuwa "chaguo la kihistoria"
Mzozo wa Ukraine yumkini ndiyo sababu ya kura ya ´Ndiyo´
Kura hiyo ya maoni imefanyika katika wakati mataifa jirani na Denmark ya Finland ana Sweden yameomba kuwa wanachama wa Jumuiya ya NATO uamuzi ambao yumkini umetokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Iliitishwa na waziri mkuu Frederiksen ndani ya wiki mbili tu baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine baada ya kupata uungwaji mkono na vyama vyote vikubwa katika bunge la Denmark, Folketing.
Kiongozi huyo pia alitangaza kuongeza bajeti ya ulinzi kufikia asilimia 2 ya pato jumla la ndani ifikapo mwaka 2033 ili kuendana na malengo ya Jumuiya ya Kujihami, NATO, ambayo Denmark ni miongoni mwa wanachama.