Deniz Yücel siku 365 jela na zahma dhidi ya SPD magazetini
14 Februari 2018Tunaanzia Uturuki ambako ripota wa gazeti la die Welt Deniz Yücel anashikiliwa kizuwizini tangu mwaka mmoja uliopita, bila ya kufikishwa mahakamani. Ni "mateka wa kisiasa" wanasema wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika: "Siku 365 bila ya kufunguliwa mashitaka. Mwandishi habari wa kijerumani mwenye asili ya Uturuki, Deniz Yücel yuko jela nchini Uturuki tangu mwaka mmoja uliopita. Kushikiliwa kwake jela si chochote chengine isipokuwa utekaji nyara wa kisiasa. Na hali hiyo inashuhudiwa pekee katika nchi zenye tawala za kiimla mfano wa Korea ya Kaskazini. Kadhia ya mwandishi habari huyu si tukio la kipekee. Kwa mujibu wa shirika la "Maripota wasiokuwa na Mipaka" , waandishi habari zaidi ya 100 wamekamatwa nchini Uturuki tangu njama iliyoshindwa ya mapinduzi. Juhudi za kila aina zinaendeshwa kupigania waachiliwe huru, tangu kidiplomasia, kisiasa mpaka kupitia mashirika ya raia. Kesho alkhamisi Angela Merkel atajipatia tena fursa ya kuzidisha shinikizo la kisiasa kwa Uturuki, atakapokutana na waziri mkuu Binali Yildirim mjini Berlin. Hadi wakati huu serikali ya Merkel ilipinga mbinu zote za kufikia maridhiano katika suala hilo na bora hivyo."
Zahma zagubika chama chab SPD
Dhoruba ya kisiasa inayokitikisa chama cha Social Democrat cha Ujerumani SPD haijatulia licha ya kuteuliwa kiongozi wa mpito kuambatana na madai ya baadhi ya wanachama wa mashinani. .Gazeti la "Berliner Zeitung" linaandika: "Lawama kutoka matawi kadhaa ya SPD dhidi ya mpango wa kumkabidhi kwa muda Andrea Nahles , wadhifa wa mwenyekiti wa chama hicho, zilikuwa za haki. Kila kitu kinaashiria bibi Nahles atakuwa mwanasiasa mwenye nguvu kabisa katika chama hicho. Lakini mbinu alizotumia hazikuwa za busara na zimemharibia. Andrea Nahles anabidi ajifunze kutokana na makosa aliyofanya kabla ya kukabidhiwa wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha SPD. Wanachama wengi wa SPD wamechoshwa na mitindo ya viongozi kuteuliwa kichini chini."
Mageuzi ya kina yanahitajika
Gazeti la Pforzheimer Zeitung linaashiria SPD wanajichimbia kaburi lao wenyewe. Gazeti hilo linaendelea kuandika: "SPD wanajichimbia wenyewe kaburi lao. Na hapo hakuna, si Angela Merkel, si GroKo na wala si yoyote mwengine wa kulaumiwa. Isipokuwa wao wenyewe. Andrea Nahles pia atatumbukia akiwa mwenyekiti wa chama. Maridhiano ya kiujanja ujanja ya kumteuwa Olaf Scholz awe mwenyekiti wa muda hadi mkutano mkuu utakapoitishwa hayatasaidia pakubwa. Nahles angebidi akabiliane na kura ya wanachama. La sivyo na yeye pia ataangaliwa kuwa ufumbuzi wa muda. Na hali hiyo itazifanya zahma zinazokigubika chama cha SPD zizidi makali.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga