Demokrasia Afrika Mashariki mashakani - Wasomi EAC
10 Oktoba 2017Wajumbe hao wanasema kinachoshuhudiwa katika nchi wanachama ni jambo lisilofaa kutokana na hali ya matumizi ya mabavu na nguvu katika kuminya uhuru wa kujieleza na uzingatiajia wa utawaLa unaoheshimu sheria na katiba za nchi.
Wajumbe hao wametoa mifano mbalimbali katika nchi wanachama na kusema hakuna taifa lolote mwanachama wa muungano huo ambaye anaonekana kuzingatia dhana ya kweli ya utawala bora na demokrasia.
"Kimsingi kinachoonekana ni kukanyagwa kwa Ibara ya Sita ya mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichowekwa miaka 14 iliyopita," wanahoji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo na Sera barani Afrika (FORDIA), Buberwa Kaiza, amesema kuwa mataifa mengi ya Afrika yameshindwa kuweka ustaarabu wa dola wanazoziongoza na ndio maana "majeshi na polisi yamekuwa yakionekana kutumia nguvu kubwa kuzima kelele za wananchi wanaodai demokrasia na utawala bora."
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa mkutano huo wenye maudhui yanayosisitiza demokrasia na utawala bora kama msingi wa kufikiwa kwa maendeleo endelevu ya jumuiya hiyo una jukumu la kuangazia changamoto zinazoshuhudiwa katika nchi wanachama na kusisitiza juu ya "uwepo wa demokrasia ya kweli na utawala bora katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Vijana waona matumaini yapo
Pamoja na suala la demokrasia kutiliwa mashaka katika nchi za Afrika Mashariki, baadhi ya vijana wanaohiudhuria mkutano huo kuwakilisha kundi la vijana wanasema kuwa hata kama hali sii shwari, bado kuna upenyo.
"Bado kuna matumaini ya kufikiwa kwa demokrasia na utawala bora katika nchi za Afrika Mashariki," anasema Umar Musa, kijana kutoka Uganda akiwakilisha kundi la Mabalozi wa Afrika Mashariki
Naye naibu katibu mkuu wa Jumuiya hiyo anayeshughulikia suala la kufikiwa kwa shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki, Charles Njoroge, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo alisema kuwa kutofikiwa kwa viwango bora katika demokrasia na utawala bora "kumekuwa chanzo cha migogoro na vita na kusababisha ongezeko la umasikini."
Njoroge aliongeza kuwa "demokrasia na utawala bora ni suala mtambuka", lenye umuhimu wa kungaziwa wakati jumuiya hiyo ikiendelea na harakati za kuelekea kuwa shirikisho la kisiasa katika siku za usoni.
Mkutano huo unahudhiuriwa na watendaji wa vyombo vya mahakama, sheria,utawala, bunge na watendaji wa sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwandishi: Charles Ngereza/DW Arusha
Mhariri: Mohammed Khelef