Democratic waanza mkutano mkuu
4 Septemba 2012Miaka 12 iliyopita, Barack Obama alihutubia mkutano wa kumpitisha mgombea urais wa Marekani kwa chama cha Democratic, John Kerry. Miaka minne baadaye ni yeye aliyekuja kupitishwa na mkutano huo, na Alhamis ya kesho kutwa (6 Septemba 2012) anatarajiwa kupitishwa tena kutetea kiti hicho.
Hadi sasa, kura za maoni zinaonesha kuwa tafauti kati ya Obama na Mitt Romney wa Republican ni ndogo sana, licha ya kwamba Obama anatajwa kuongoza. Timu ya kampeni ya Obama imetumia kila njia za kisasa na kongwe, kuhakikisha kuwa mgombea wao anaaminiwa tena na Wamarekani.
Mfano ni tangazo hili kutoka kwa rais wa zamani, Bill Clinton, ambaye kama alivyo Obama, naye pia anatokea Democratic, ambapo Cliton anamsifu Obama kuwa na mipango ya kujenga tabaka la kati lenye nguvu kwa ajili ya uwekezaji, elimu na ajira, huku Romney akikusudia kuwanyima fursa watu wa tabaka hilo kwa maslahi ya matajiri wachache.
Kuwepo kwa Clinton kwenye mkutano huo wa siku tatu unaofanyika katika mji wa Charlotte, North Caroline, kunatazamiwa kuongeza kiwango cha Obama kuungwa mkono.
Kazi ngumu kumnadi Obama?
Democratic inakabiliwa na kazi ngumu ya kuwashawishi wapiga kura katika wakati ambapo rikodi ya ukosefu wa ajira ikiwa asilimia 8.3. Matukio makubwa yanayotazamiwa kwenye mkutano huu, ni pamoja na hotuba ya mwenyewe Rais Obama hapo Alhamis, wakati akikubali uteuzi wa chama chake.
Hiyo ni hotuba inayotarajiwa kujenga hoja kwamba hata baada ya miaka minne ya kuwapo madarakani na kufeli kwa uchumi, bado yeye ndiye mwenye uwezo wa kuinusuru hali na kulifanya taifa hilo kubwa kabisa duniani kusonga mbele. Obama atawaambia wapiga kura kuwa Marekani iko salama zaidi mikononi mwake, kuliko kwenye mikono ya Romney.
Hadi sasa, hotuba nyingi za Obama zinaonekana kujikita zaidi kuonesha kwa nini Obama anaamini Romney hachaguliki, kuliko kuelezea mbinu zake mahsusi kupambana na ukosefu wa ajira na kuziba mwanya wa nakisi ya bajeti.
Ujumbe mzito wa Obama unatarajiwa kuwa ni ule wa kuiinua uchumi kutoka chini kwenda juu, kwa kuzisaidia familia za tabaka la kati na kukatisha nafuu ya kodi kwa matajiri. Kwa kuzungumza kauli za wazi zaidi kuliko mwenzake Romney, ambaye anakosolewa kwa kutumia nafasi kama hiyo wiki iliyopita.
Obama amponda Romney
Katika matangazo yake ya kampeni, tayari Rais Obama ameshachora mstari baina yake na Romney, akisema kwamba uchaguzi huu "si kati ya vyama viwili vya siasa au wagombea wawili tu, bali kati ya mipango miwili tafauti ya kuendesha nchi."
Obama anatarajiwa kutumia masuala kama vile kupitishwa kwa sera yake ya bima ya afya, maarufu kama Obamacare, na pia kuuawa kwa Osama bin Laden na majeshi ya Marekani, kama alama za mafanikio yake ndani na nje ya Marekani.
Kwa sasa Rais Obama yuko kwenye ziara ya siku nne inayojuilikana kama "Barabara Kuelekea Charlotte" katika jimbo ambalo litaamua hasa mshindi katika uchaguzi wa Novemba.
Tayari ameshatembelea majimbo ya Iowa, Colorado na jiimbo lililoathirika sana kwa kimbunga la Lousiana. Ikiwa Obama atashinda Ohio, kuna uwezekano mkubwa sana akapata tena nafasi ya kubakia Ikulu ya Marekani, kwani hakujawahi kuwapo mwanachama wa Republican aliyeshinda urais, bila ya kwanza kushinda Ohio.
Jumanne (4 Septemba 2012) Obama alitembelea jimbo jingine lenye wapiga kura ambao hawajaamua, Virginia, kabla ya hapo kesho kusafiri kwa ndege kuelekea Charlotte, North Carolina, kwa ajili ya mkesha wa hotuba yake inayosubiriwa kwa hamu, ndani na nje ya Marekani.
Akiwahutubia wafuasi wake mjini Colorado siku ya Jumapili, Obama alimkosoa Romney kwa "kushindwa kuja na hata mbinu moja mpya ya kutatua matatizo ya kiuchumi yanayoikabili Marekani", ambayo wafuasi wa Democrat wanadai kwamba yalitengenezwa wakati wa miaka minane ya utawala wa George Bush kutoka Republican.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf