Dembele atambulishwa Barcelona
28 Agosti 2017Utambulisho wa chipukizi wa Kifaransa Ousmane Dembele kama nyota mpya kabisa wa Barcelona umegubikwa na hali ya wasiwasi inayoikabili klabu hiyo wakati mashabiki walipiga kelele na kumzomea rais Josep Maria Bartomeu wakimtaka ajiuzulu.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 amekuwa mchezaji wa pili mwenye gharama kubwa kabisa duniani baada ya kukamilisha siku ya Ijumaa uhamisho wake kutoka Borussia Dortmund wa euro milioni 105, kiasi ambacho kinaweza kupanda hadi milioni 147 katika malipo mengine ya ziada.
Hata hivyo, ratiba iliyopangwa ya Barca ya uzinduzi huo mkubwa ilicheleweshwa kwa karibu saa mbili kutokana na suala la nyaraka katika kumsajili Dembele kutoka Dortmund. Karibu mashabiki 18,000 waliofika Camp Nou walipiga kelele wakati wa kucheleweshwa huko wakisema kwa sauti kubwa "Bartomeu jiuzulu”.
Bodi ya Barca imekuwa chini ya shinikizo baada ya uhamisho wa Neymar ulioigharimu PSG euro milioni 222.
Akiwa amevalia jezi namba 11 iliyoachwa na Neymar, Dembele amewaambia mashabiki, ana furaha kujiunga na Barca. "ni klabu bora duniani na ina wachezaji bora duniani”. Alisema.
Dembele ataunda kikosi cha kuogofya cha safu ya mashambulizi pamoja na mchezaji bora wa mwaka mara tano Lionel Messi na Luis Suarez wakati Barca ikilenga kuwapokonya mahasimu wake Real Madrid taji la La Liga.
Kule alikotoka, atakayevaa njumu zake kapatikana. Dortmund imetangaza leo kuwa imemsajili Andrey Yarmolenko kutoka Dynamo Kiev ya Ukraine kuchukua nafasi ya Dembele.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Abdulrahman