Dedan Kimathi alikulia katika mazingira gani?
Dedan Kimathi alizaliwa Kimathi wa Waciuri Oktoba 31, 1920 katika kijiji cha Thege karibu na Nyeri katikati mwa Kenya. Alianza shule ya msingi akiwa na umri wa miaka 15 na baade kujiunga na shule ya sekondari ya Church of Scotland Mission, lakini alitoroka kabla ya kumaliza masomo yake.
Kimathi alipata elimu yake ya msingi kipindi cha ukoloni katika mazingira magumu. Baba yake alifariki kabla hajazaliwa. Hata hivyo, rekodi zake zinaonyesha alikuwa mwanafunzi hodari. Alifaulu zaidi kwenye somo la lugha ya Kiingereza na mashairi na alikuwa mshiriki mkubwa wa klabu ya mjadala shuleni.
Ingawa Kimathi alikuwa hodari darasani, lakini pia akijulikana kwa utundu na ukaidi. Baadhi ya wanahistoria wanadai tabia yake ya uasi sio kwa sababu ya chuki dhidi ya utawala wa watu weupe lakini ni kutokana na kutendewa vibaya na watu weusi. Watoto wenzake aliokuwa akicheza nao walimpa jina la utani la Kikuyu la ‘Njangu’ linalomaanisha tapeli. Hatimaye alifukuzwa shule mnamo mwaka 1944 kwa kukosa nidhamu darasani.
Dedan Kimithi alitoka kabila gani?
Kimathi alitoka katika ukoo wa Ambui, moja ya koo nyingi zinazounda kabila la Kikuyu, ambalo ni kubwa zaidi nchini Kenya na watu wake wengi wnaishi katikati mwa Kenya. Jomo Kenyatta, rais wa kwanza wa Kenya, alitokea katika kabila la Kikuyu. Kuna wanahistoria wanadai kwamba Kenyatta na Kimathi hawakuwa na mtazamo sawa kwenye suala la kupigania uhuru wa Kenya. Kenyatta alipendelea kutumia mbinu isiyo na vurugu, Kimathi kwa upande wake aliamini kutumia bunduki ndiyo njia pekee ya kuikomboa Kenya.
Ilikuwaje hata Dedan Kimathi akawa mpigania uhuru?
Kama kijana, Kimathi alijaribu bahati kwa kufanya kazi mbalimbali. Aliwahi kuwa karani, alichunga nguruwe pamoja na kufundisha. Kutokana na uwezo wake mzuri wa kuzungumza kugha ya Kiingereza, ilikuwa rahisi kwake kupata kazi tofauti. Lakini pia wakati huo huo alianza kuchoshwa na jinsi wakoloni wanavyoitawala na kuiendesha nchi.
Mnamo mwaka 1951, Kimathi aliungana na wapigania uhuru wengine nchini Kenya wa vuguvugu ambalo baade lilikuja kujulikana kama Mau Mau. Haraka alipanda safu na kupewa kazi ya kuwalisha kiapo wanachama wapya wa vuguvugu hilo. Mnamo 1952, wakati utawala wa Uingereza ulipotangaza hali ya hatari, Kimathi alikimbilia msituni karibu na Mlima Kenya.
Alikuwa miongoni mwa wapiganaji watatu wanaoogopewa zaidi wa vuguvugu liko la kupigania uhuru wa Kenya. Alikuwa mmoja wa viongozi wa kitengo kilichoitwa Baraza la Ulinzi la Kenya. Aliandaa mashambulizi ya silaha dhidi ya serikali ya wakoloni ya Uingereza.
Nini chimbuko la Mau Mau?
Mau Mau ni vuguvugu liloanzishwa kwa lengo la kuwafurusha walowezi wa Uingereza waliokamata kwa nguvu ardhi ya Wakenya. Awali, wapiganaji wa Mau Mau walikuwa ni kutoka kabila la Kikuyu, ambao ardhi yao ilipendelewa zaidi na walowezi wa Kizungu, lakini baadae, Meru, Embu, Kamba na makabila mengine yalijiunga na harakati hizi za uhuru.
Haijulikani hakika lilipotokea jina la Mau Mau. Wengine wanasema linatokana na neno la Kikuyu ‘uma’ linalomaanisha, ‘nenda’. Hata hivyo, wanachama wa vuguvugu hilo wakipendelea kuitwa kwa jila la Jeshi la kupigania Ardhi na Uhuru wa Kenya (KLFA). Baadae jina la Mua Mau lilikuja kujulikana kama: ‘Mzungu arudi Ulaya, Mwafrika apate uhuru’.
Wapiganaji walikula kiapo kilichowalazimisha kukubaliana na malengo ya vuguvugu hilo. Wanachama kadhaa wa zamani baadaye walizungumzia uandikishwaji wa nguvu. Vuguvugu hilo lilikuwa likiwatia hofu walowezi wa Uingereza pamoja na Waafrika wenye misimamo ya wastani, ambao waliwalenga kwa madai ya kusaliti harakati za ukombozi na badala yake kushirikiana na walowezi.
Watu wangapi waliuawa wakati wa mapambano ya Mau Mau?
Rekodi rasmi katika Jalada la Kitaifa la Kenya zinaonyesha kwamba Wakenya zaidi ya 10,000 waliuawa mikononi mwa vikosi vya usalama vya wakoloni wa Uingereza na karibu 50,000 walishikiliwa vizuizini baada ya utawala wa kikoloni kutangaza Hali la Dharura mnamo Oktoba 1952. Serikali ya kikoloni ya Uingereza pia ilitekelezea mauaji 1,090. Kwa upande mwingine, mamia ya watu, wengi wao wakenya, walidaiwa kuuawa na wapiganaji wa Mau Mau.
Kifo cha Dedan Kimathi kilitokea vipi na amezikwa wapi?
Mnamo Oktoba 21, 1956,Dedan Kimathi aliyejitangaza kama jenerali wa kijeshi wa vuguvugu la Mau Mau alikamatwa katika msako uliokuwa ukiongozwa na Ian Henderson, afisa wa kijasusi wa Uingereza. Lakini hakuwa Henderson aliyemkamata Kimathi mwanzo. Alikamatwa baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa Kikenya anayetoka katika kabila moja naye la Kikuyu.
Haraka, Kimathi alifunguliwa kesi na hatimaye kuhukumiwa adhabu ya kifo iliyotekelezwa Febuari 18, 1957. Wakoloni waliuzika mwili wake kwenye kaburi ambalo halikuwekwa alama yoyote katika Gereza la Kamiti la Ulinzi Mkali, kusudi ili Wakenya wasijeanzisha mazoea ya kulitembelea kaburi la mpigania uhuru huyo.
Kwa miongo kadhaa baadae, wanafamilia wa Kimathi, jamaa na serikali ya Kenya waliiomba Uingereza kuwaeleza alipozikwa Kimathi lakini bila ya mafanikio yoyote. Mwaka 2019 ndipo eneo lilipo kaburi lake lilipowekwa wazi.
Dedan Kimathi anakumbukwa vipi?
Kuna barabara moja jijini Nairobi iliyopewa jina la Dedan Kimathi. Na 2007, rair wa zamani wa Kenya Mwai Kibaki alizindua sanamu la shaba la Kimathi lenye urefu wa mita mbili ambalo limewekwa kwenye barabara hiyo hiyo iliyopewa jina lake. Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Kimathi na Uwanja wa Dedan Kimathi huko Nyeri ni miongoni mwa taasisi kadhaa zilizopewa jina la mpiganaji huyo mashuhuri wa vuguvugu la Mau Mau.
Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.