1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deby mwenyekiti mpya Umoja wa Afrika

30 Januari 2016

Rais wa Chad Idriss Deby amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika, akichukuwa nafasi ya rais wa Zimbabwe Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/1HmIF
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika Rais Idriss Deby wa Chad.
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika Rais Idriss Deby wa Chad.Picha: Thierry Charlier/AFP/Getty Images

Uteuzi wake huo umefanyika wakati viongozi wa Afrika wakikutana Jumamosi(30.01.2016) katika juhudi za kukomesha mizozo yenye kuhusisha matumizi ya silaha ukiwemo ule wa Burundi ambapo wanatazamiwa kupiga kura isio na kifani ya kutuma wanajeshi wa kulinda amani nchini humo licha ya upinzani mkali wa nchi hiyo.

Akikubali uteuzi huo kwa kile alichosema ni furaha iliyochanganyika na maumivu kutokana na uzito wa changamoto zinazoukabili umoja huo, Deby amesema migogoro lazima ikome barani Afrika.

Amesema kila wanachokifanya sasa hakitakuwa na maana yoyote na ikiwa wataruhusu migogoro kushamiri barani Afrika, na kuitaja baadhi ya migogoro hiyo inayoendelea katika mataifa ya Sudan Kusini, Libya, Somalia, Burundi, eneo la Sahel, na ukanda wa ziwa Chad.

Mshirika muhimu dhidi ya Boko Haram

Deby mwenye umri wa miaka 63, na mmoja wa watawala wa muda mrefu barani Afrika, aliingia madarakani Desemba1990 kufuatia vita vilivyoangusha utawala wa Hissene Habre.

Wanajeshi wa Nigeria katika mapambano na Boko Haram.
Wanajeshi wa Nigeria katika mapambano na Boko Haram.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Kiongozi huyo amekuwa mshirika muhimu kimkakati katika mapambano dhidi ya magaidi wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria na katika kanda hiyo.

Mtangulizi wake Mugabe mwenye umri wa miak 91, alieshikilia wadhifa huo usiyo wa kiutendaji na wa kupokezana katika umoja huo, amemuahidi Deby msaada wowote atakaohitaji madamu yuko hai.

Suala Burundi kuhodhi agenda

Wakati mada rasmi katika mkutano huo ni suala la haki za binaadmu viongozi hao kwa mara nyengine tena wanakabiliwa na mkururo wa mizozo barani humo wakati wa mkutano wao wa siku mbili katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Machafuko nchini Burundi.
Machafuko nchini Burundi.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Mazungumzo katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yaliohudhuriwa na marais na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama 54 wa umoja huo yaliendelea hadi wa usiku wa manane Ijumaa katika juhudi za kupunguza tafauti zao na kuwa na misimamo ya pamoja kabla ya kuanza rasmi kwa mkutano huo Jumamosi.

Mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma ameufunguwa mkutano huo wa kilele kwa kuwakumbuka walinda amani wa Umoja wa Afrika waliouwawa katika juhudi za kunyamazisha mapigano huku kukiwa na mdahalo mkali wa kupeleka kikosi kipya nchini Burundi.

Suala la kutuma vikosi mashakani

Baadhi ya mataifa ya Afrika yanapinga kutumwa kwa kikosi hicho nchini Burundi bila ya ridhaa ya serikali ya nchi hiyo baada ya rais wa nchi hiyo kusema hatua hiyo itachukuliwa kama uvamizi wa nchi hiyo.

Wanajshi wa Umoja wa Afrika wakiwa kazini.
Wanajshi wa Umoja wa Afrika wakiwa kazini.Picha: picture alliance/dpa/Jones

Hapo mwezi wa Disemba Baraza la Amani na Usalama la umoja huo lilitangaza mpango wa kupeleka kikosi cha wanajeshi 5,000 katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati ambapo mamia ya watu wameuwawa katika machafuko mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo tokea kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe chini ya misingi ya kikabila hapo mwaka 2005.

Suala la Burundi limepewa kipau mbele kikubwa katika agenda ya mkutano huo wa kilele wa siku mbili kutokana na ongezeko la matumizi ya nguvu kuitingisha kanda nzima ya Afrika ya Kati ambayo ina historia ya mizozo ya kikabila.Mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda yameuwawa watu 800,00.

Gambia yapinga kutuma vikosi Burundi

Rais Yahya Jammeh wa Gambia amesema sio Burundi tu inayopinga wazo la kutuma vikosi.Alikuwa akijibu suali iwapo kuna upinzani kwa mpango huo wa kutuma walinda amani.Hata hivyo hakutaja mataifa yanayopinga mpango huo.

Rais Yahya Jammeh wa Gambia.
Rais Yahya Jammeh wa Gambia.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Jammeh ambaye nchi yake ni mwanachama wa Baraza la Amani na Usalama la nchi 15 amesema hatounga mkono kutumwa kwa kikosi hicho bila ya ridhaa ya Burundi.

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele mwanadiplomasia mmoja wa Afrika ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba Misri nchi nyengine mwanachama wa baraza hilo pia ina mashaka na kuwekwa kwa kikosi hicho. Maafisa wa serikali ya Misri hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.

Zinahitajika theluthi mbili ya kura kutuma kikosi hicho kitakachojulikana kwa jina la (MAPROBU) cha kuzuwiya machafuko na kulinda raia. Haijulikani nani atakuwa tayari kuchangia wanajeshi katika kikosi hicho.

Rais Piere kushawishiwa

Maafisa wamesema viongozi wa Afrika katika mkutano huo watajaribu kumshawishi Rais Piere Nkurunziza ambaye ndie aliechochea mzozo huo kutokana na kuwania muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi wa mwezi wa Julai akubali kupelekwa kikosi hicho.Lakini pia wamesema hawadhani watafanikiwa kwa hilo.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi.Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

"Linapokuja suala la vikosi, msimamo wetu haukubadilika ni mahala kusikoruhusiwa kupelekwa vikosi katika mazingira yoyote yale." Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Alain Nyamwite amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa.

Iwapo Umoja wa Afrika itapeleka kikosi hicho bila ya ridhaa ya Burundi itabidi itumie ibara ya nne ya katiba ya Umoja wa Afrika ambayo inaruhusu kuingilia kati katika nchi mwanachama iwapo hali ni mbaya sana kama vile: uhalifu wa kivita,mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litatakiwa litowe idhini ya mwisho.

Ban ataka kuwajibishwa viongozi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon ameonya kwamba "viongozi wanaokaa pembeni bila ya kuchukuwa hatua wakati wanachi wakiuwawa kwa majina yao lazima wawajibishwe."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon akizungumza mjini Addis Ababa katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika. (29.01.2016)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon akizungumza mjini Addis Ababa katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika. (29.01.2016)Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Amesema mzozo wa Burundi unahitaji kujitolea kwa nia na kwa haraka."

Pia amesema kwamba Umoja wa Mataifa unaunga mkono pendekezo la Umoja wa Afrika kutuma waangalizi wa haki za binaadamu na kikosi cha kuzuwiya machafuko na kulinda raia nchini Burundi.

Zuma anamaliza muda wake

Suala jengine lilioko juu kwenye agenda ni uchaguzi wa mkuu mpya wa kamisheni ya Umoja wa Afrika kwani kipindi cha kiongozi wa sasa Nkosazana Dlamini Zuma kutoka Afrika Kusini kinamalizika mwaka huu.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma.
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma.Picha: Simona Foltyn

Mke huyo wa zamani wa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini mwenyewe anaumezea urais wa nchi yake na hiyo inamaanisha kwamba hatogombea kipindi kengine katika wadhifa huo.

Mojawapo wa wagombea mashuhuri anayewania nafasi hiyo ni waziri wa mambo ya nje wa Algeria Ramtane Lamamra ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2013.Iwapo atafanikiwa atakuwa mtu wa kwanza kushika wadhifa huo kutoka Afrika Kaskazini.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters /AFP

Mhariri :Iddi Sessanga