De Maziere afanya ziara ya ghafla Afghanistan
22 Desemba 2011Matangazo
De Maziere amesema kuwa hali ya usalama nchini Afghanistan imeimarika kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa. Matukio yanayohatarisha usalama yamepungua kwa asilimia 25 katika nchi hiyo na asilimia 50 kwa eneo la kaskazini. Waziri huyo wa Ulinzi amesindikizwa na kamati ya ulinzi ya Bunge la Ujermani na pia kamishna wa Bunge wa Vikosi vya Ulinzi, Hellmut Königshaus.
Hivi karibuni, jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) lilikabidhi kituo cha kwanza cha kijeshi kwa serikali ya Afghanistan, ikiwa ni hatua ya kwanza kuelekea kujiondoa kabisa kijeshi nchini humo. Kwa sasa Ujerumani ina wanajeshi 5,000 wanaotumika kwenye kikosi cha kimataifa cha walinda amani Kaskazini mwa Afghanistan. Wanajeshi 1,200 kati ya hao wako mjini Kunduz.