De Maizière ajitetea mbele ya wabunge
31 Julai 2013Waziri de Maizière ametetea uamuzi wake wa kuusimamisha mradi wa kununua ndege aina ya Euro Hawk na kukanusha madai yote yanayomkabili. Katika tamko alilolitoa mbele ya kamati maalum ya uchunguzi ya bunge, de Maizière alisisitiza kwamba tangu Machi mwaka jana, alifahamu kwamba ndege za Euro Hawk zinaweza kupata tatizo la kutokusajiliwa. Hata hivyo ameeleza kuwa aliamini tatizo hilo lingeweza kusuluhishwa. De Maizière aliongeza kwamba gharama za kupata kibali ziliongezeka Mei mwaka huu na hapo ndipo katibu mkuu wa wizara yake alipoamua kutokununua ndege hizo.
Hata hivyo, kamati ya uchunguzi bado haijakubaliana na maelezo ya waziri huyo ya kwamba alichelewa kupata taarifa muhimu juu ya ubora wa ndege hizo pamoja na gharama za ununuzi. Joachim Spatz ni mwanasiasa wa chama cha FDP kinachounda serikali pamoja na chama cha CDU.
"Waziri alipewa nyaraka zote mwezi Disemba mwaka jana. Nyaraka hizo zinaelezea kwa kina matatizo ya Euro Hawk pamoja na hatari zinazoambatana na ununuzi wa ndege hizo," alisema Spatz. "Kwahiyo alifahamu yote hayo na akaamua kusema uongo. Ninajiuliza iwapo mtu kama huyo anastahili kuendelea kuwa waziri."
Hasara ya mamilioni
Uamuzi wa kuagiza ndege zisizo na rubani ulipitishwa mwaka 2001. Mpaka sasa, utengenezaji wake umegharimu zaidi ya Euro milioni 600 na inaonekana kwamba serikali ya Ujerumani italazimika kulipa fedha nyingi zaidi ili ndege hizo zipate kibali cha kuruka angani.
Akijitetea mbele ya kamati ya uchunguzi, de Maizière alikumbusha kwamba yeye aliteuliwa kuwa waziri wa Ulinzi mwaka 2011. Wakati huo, zaidi ya asilimia 85 ya bajeti ya kuagiza ndege hizo ilikuwa imeshatumika.
De Maizère hataki kujiuzulu
"Markus Grübel ambaye ni mjumbe wa kamati ya uchunguzi wa bunge kutoka chama tawala cha CDU amesisitiza kwamba de Maiziere hakufanya kosa lolote.
Mpaka sasa mashahidi wote wamedhihirisha kwamba waziri hakumbwi na hatia yoyote. Shutuma za upande wa upinzani zinaonekana kuwa za uongo," alisema Grübel.
Alipoulizwa kama amefikiria kujiuzulu, de Maizière alisema hapana. Uchaguzi mkuu hapa Ujerumani unafanyika mwezi Septemba. Iwapo de Maizière atalazimika kujiuzulu, hilo litakuwa pigo kubwa kwa Kansela Angela Merkel ambaye ameshuhudia mawaziri kadhaa wakijiuzulu katika kipindi cha utawala wake.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf