Dday ni operesheni iliyotuondolea wanazi Ujerumani-Merkel
5 Juni 2019Viongozi mbali mbali wa dunia akiwemo rais wa Marekani Donald Trump walijiunga na Malkia Elizabeth wa Uingereza kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 75 tangu zilipofanyika harakati kubwa za aina yake za kijeshi zilizokuja kuikombowa Ulaya katika vita vya pili vya dunia dhidi ya Wanazi wa Ujerumani,katika kile kinachoitwa DDay.
Viongozi wakuu wa nchi mbali mbali duniani akiwemo rais wa Marekani na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel walikuwepo kwenye kumbukumbu hizo za kihistoria ambapo kwa pamoja na malkia wa Uingereza walitowa pongezi za binafasi kwa wakongwe walioshiriki katika vita vya pili vya dunia waliohudhuria tukio hilo.
Uvamizi wa kijeshi wa DDay ni harakati zilizofanyika miaka 75 iliyopita zikihusisha wanajeshi wa nchi mbali mbali zilizopigana bega kwa bega na Uingereza dhidi ya Ujerumani kusaidia kumaliza vita vya pili vya dunia.
Malkia Elizabeth,mwanamfalme Charles,marais na mawaziri wakuu walisimama mbele ya jukwaa kubwa kando ya gwaride la heshima la kijeshi baada ya kuoneshwa filamu kuhusu tukio la jinsi wanajeshi walivyotuwa Normandy nchini Ufaransa katika harakati hizo za kuikomboa ulaya mwaka 1944. Malkia Elizabeth wa pili mwenye umri wa miaka 93 akiwa amevalia nguo rangi ya pinki ya kukoza alisikika akisema na hapa tunanukuu'' kizazi cha wakati wa vita,yaani enzi zangu tumehimili mengi na ninafuraha kuwa nayni hapa Potsmouth leo hii.
Kadhalika ameongeza kusema kwamba ujasiri uthubutu na kujitolea kwa wale waliopoteza maisha yao ni jambo halitosahaulika katu. Na kwa niaba ya Uingereza na dunia kwa ujumla amewashukuru wanajeshi hao waliopambana.Waziri mkuu Theresa May aliungana pia katika sherehe za kumbukumbu hiyo na rais Donald Trump ambaye yuko kwenye siku yake ya mwisho ya ziara yake nchini Uingereza. Rais Trump alisoma risala ya dua iliyotolewa na Franklin D Roosevelt mwaka 1944 inayosema,''Adui ana nguvu. Anaweza kuvirudisha nyuma vikosi vyetu lakini tutarudi tena na tena,na tunafahamu kwamba kwa uwezo na uthabiti wetu,watoto wetu watashinda'.Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema.DDay ni tukio la kipekee la kijeshi ambalo hatimae liliondolea Ujerumani utawala wa wanazi na lilihusisha wengi kujitolea maisha yao,mamia kwa maelfu ya wanajeshi kuuwawa na juhudi nyingine nyingi.Lakini pia ni siku ya kujivunia kwa kuleta maridhiano,mshikamano,na umoja ndani ya Ulaya lakini pia kujenga kanuni baada ya vita ambazo zimeleta amani kwa zaidi ya miongo saba''
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron,waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau,waziri mkuu wa Australia Scott Morrison,kansela Angela Merkel na viongozi pamoja na maafisa wa ngazi ya juu kutoka nchi nyingine 10 pia walihudhuria. Jini leo wakongwe 300 waliopigana vita ambao kwasa sasa wana umri wa zaidi ya miaka 90 wataondoka Portsmouth kwa meli maalum inayoitwa MV Boudicca na kufanya safari kama ya mwaka 1944 wakisindikizwa na meli za jeshi la wanamaji la Uingereza na ndege za kivita.Matukio mengine ya kumbukumbu hiyo yatafanyika pia kesho kaskazini mwa Ufaransa.
Ikumbukwe kwamba Juni 6 1944 vikosi vya muungano wa wanajeshi 150,000 walioondoka katika pwani ya Portsmouth kuanza mashambilizi ya angani,baharini na ardhini dhidi ya wanazi huko Normandy,Ufaransa,mapambano ambayo yalipelekea hatimae ukombozi wa Ulaya ya Magharibi kutoka mikononi mwa utawala wa wanazi wakijerumanil.Ni operesheni iliyohusisha takriban meli 7000 za kijeshi na madege yakivita katika eneo hilo la pwani ya Ufaransa.Maelfu waliuwawa kutoka kila upande.