1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

David Cameron kujibu maswali ya wabunge leo

20 Julai 2011

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron atahojiwa na bunge leo kuhusiana na uamuzi wake wa kumuajiri mhariri wa zamani wa gazeti la News of the World ambaye anahusishwa na kashfa ya unasaji mawasiliano ya simu.

https://p.dw.com/p/12041
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron,anakabiliwa leo na maswali bungeni juu ya kashfa ya unasaji mawasiliano ya simu nchini Uingereza.Picha: dapd

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron atahojiwa na bunge leo juu ya uamuzi wake wa kumwajiri mhariri wa zamani wa gazeti la News of the World , ambaye anahusishwa na kashfa ya unasaji wa mazungumzo ya simu ambayo imeiitikisa Uingereza.

►Kashfa hiyo , inayohusisha himaya ya vyombo vya habari duniani vya tajiri mkubwa Rupert Murdoch ya News Corp, imesababisha kujiuzulu kwa watendaji wa ngazi ya juu wa kampuni hilo pamoja na viongozi wa ngazi ya juu wa polisi nchini Uingereza pamoja na kuchochea mashambulio ya upande wa upinzani kuhusiana na uamuzi wa waziri mkuu David Cameron. Murdoch mwenye umri wa miaka 80 alishambuliwa na mtu mmoja aliyekuwa katika kundi la waandamanaji wakati alipofika katika jengo la bunge kuhojiwa na kamati ya bunge jana na kuomba msamaha kutokana na kashfa hiyo lakini amekataa kujiuzulu. Amesema kuwa wafanyakazi , ambao wamemsaliti wanamakosa.

Anhörung in London Murdoch
Rupert Murdoch (kulia),pamoja na mwanae James wakihojiwa katika kamati ya bunge mjini London.Picha: picture alliance/dpa

Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa samahani aliyotoa Murdoch mbele ya televisheni inamuweka sasa waziri mkuu David Cameron katika nafasi ya kutazamwa zaidi , vipi atafanikiwa katika kupambana na maswali ya wabunge katika kikao cha dharura cha bunge kuhusiana na kashfa hiyo, ambayo imejumuisha madai ya unasaji wa mazungumzo ya simu ya msichana wa shule aliyeuwawa , pamoja na simu za wanajeshi wa jeshi la Uingereza waliouwawa katika mapambano.

Mtendaji mkuu wa shirika hilo la vyombo vya habari tawi la Uingereza Rebekah Brooks alipoulizwa kuhusu unasaji wa simu ya msichana huyo aliyeuwawa, alisema nae alishutushwa sana kama watu wengine.

Bila shaka nasikitika. Wazo kwamba simu ya Milly Dowler ilinaswa na mtu ambaye amelipwa na gazeti la News of the World, ama hata kitu kibaya zaidi, iliyoidhinishwa na mtu katika gazeti hilo ni cha kuchukiza kwangu mimi kama ilivyo kwa kila mtu katika chumba hiki. Na nasikitika sana kuwa kasi ambayo tumeweza kugundua na kujaribu kugundua kiini cha uchunguzi huu imekuwa ni ndogo mno.

Rebekah Brooks
Rebekah Brooks,Mtendaji mkuu wa zamani wa News Corporation nchini UingerezaPicha: picture alliance/dpa

Saa chache kabla ya Cameron kutarajiwa kukutana na wabunge , kamati nyingine ya bunge imechapisha ripoti inayokosoa shirika hilo la News International , na tawi la Uingereza la News Corp, pamoja na polisi kuhusiana uchunguzi wa kashfa hiyo ya unasaji wa mawasiliano ya simu. Kumekuwa na mambo kadha ambayo yameshindwa kutekelezwa na polisi, na majaribio ya makusudu kwa News International kuzuwia uchunguzi katika maeneo mbali mbali, amesema Keith Vaz , mwenyekiti wa kamati ya masuala ya ndani.

Seneta wa Marekani Frank Lautenberg kutoka chama cha Democratic na Jay Rockefeller wanataka kufanyike uchunguzi , iwapo taratibu za unasaji wa mawasiliano ya simu zimetendeka pia nchini Marekani kinyume na sheria za nchi hiyo.

Sheria kwa ajili ya mashirika ya Marekani, ambapo News Corp ni mojawapo, inakataza kutumia rushwa kwa sababu yoyote ile na hapa inaonekana kuwa imetumiwa na kutokana na hayo tunataka wale ambao wanasimamia sheria kuwakamata watu hao , wachunguze na kutuambia kile kilichotokea.

Waziri wa habari Jeremy Hunt amesema kuwa News International linahitaji kujieleza jinsi hali hiyo ilivyojitokeza bila Murdoch mwenyewe ama mtoto wake James mtendaji mkuu wa News Corp kufahamishwa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri : Abdul-Rahman Mohammed◄