David Cameron afafanua malengo ya serikali yake.
12 Mei 2010Waziri Mkuu mpya wa Uingereza David Cameron, kiongozi wa chama cha Conservative, leo ameanza kazi kufuatia mapatano ya kuunda serikali ya mseto aliyofikia na kiongozi wa chama cha waliberali, Nick Clegg, hapo jana.
Serikali hiyo mpya inaingia madarakani baada ya utawala wa miaka 13 wa chama cha Labour.
Pamoja na malengo aliyofafanua ni kupunguza nakisi ya bejeti ambayo sasa imefikia asilimia zaidi ya 11 ya pato jumla la taifa.
Serikali ya waziri Mkuu David Cameron pia inatazamiwa kuutekeleza mpango wa chama chake wa kupunguza matumizi kwa kiasi cha paundi Bilioni sita mnamo mwaka huu.
Waziri Mkuu mpya huyo amesema leo kwamba serikali ya mseto aliyoiunda na chama cha Liberal Democrats inadhamiria kuwapa watu wa Uingereza uongozi imara.
Akizungumza na waandishi habari kwa mara ya kwanza leo alasiri bwana Cameron pamoja na makamu wake, Nick Clegg, alifafanua malengo ya serikali yake.
Amesema lengo mojawapo kuu ni kuipa Uingereza uongozi wenye nguvu, imara na wenye dhamira utakaohitajika kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu Cameron pia amesema mpango wa kupunguza nakisi ya serikali ni muhimu sana na kutokana na umuhimu huo serikali yake mpya imethibitisha kuwa mpango wa kubana matumizi utatekelezwa utakaookoa kiasi cha paundi Bilioni sita mnamo mwaka huu.
Serikali hiyo mpya pia itatekeleza mpango wa kupunguza idadi ya wakimbizi.
Bwana Cameron pia ameahidi kwamba ushirikiano baina ya vyama vya Conservative na Liberal Democratic utadumu kwa kipindi chote cha miaka mitano ijayo.
Wakati huo huo, majina ya mawaziri wa serikali mpya yameanza kutajwa ikiwa pamoja na la waziri wa fedha George Osborne.
Mwandishi:Mtullya abdu/AFPE/ZA.
Mhariri: Miraji Othman