Darasa la Kombe la Afrika 2008 nchini Ghana.
11 Februari 2008Kombe la Afrika la mataifa lililoanza Januari 20 mjini Accra na kumalizika juzi kwa ushindi wapili mfululizo wa 6 wa Misri baada ya kuikandika kamerun bao 1:0 limetuachia darasa gani –miaka 2 kabla ya Angola kuandaa kombe lijalo na Afrika kusini Kombe la kwanza la dunia barani Afrika ?
Hii ni mara ya 3 tu kwa mabingwa watetezi kufaulu kulitwaa tena kombe la Afrika katika historia ya kombe hili.Misri ilikuwa ya kwanza kufanya hivyo, ilipolitwaa Khartoum, 1957 na utamu ulipoikolea ikalitwaa tena nyumbani cairo,1959.Sasa baada ya kutamba nyumbani 2006 imetamba tena Accra,2008.
Simba wa nyika –kameroun ni timu ya pili kuiigiza Misri kwa kulitwaa kombe mara 2 mfululizo.
Kameroun ilitamba 2000 na ikiwa njiani kuelekea kombe la dunia 2002 huko Korea ya kusini ikatoroka nalo tena hadi Yaounde.
Inakubaliwa na mabingwa wote wa dimba kuwa kombe la 26 la Afrika sio tu limeusisimua ulimwengu kuliko yote hadi sasa na ufundi wa dimba wa timu za Afrika umeongezeka,lakini kumebainika pia kasoro katika uwezo wa bara la Afrika kimaandalio:
Afrika iliwatembeza mastadi zaidi wa dimba walioonekana dunia nzima mnamo wiki 3 zilizopita.Tumeona mchezo wa kushambulia na idadi ya magoli 99 katika mechi 32 ni ushahidi wa hayo.
Upande wa mastadi,mabingwa Misri licha ya kuwa inaegemea zaidi wachezaji wa nyumbani kutoka klabu zake 2 Al Ahly na Zamalek, imechangia wachezaji 5 katika listi ya timu bora ya Afrika kutoka kombe hili:
Wakati samuel Eto’o wa Kamerun ameibuka mtiaji mabao mengi kuliko yeyote-mabao 5 na kuivunja ile rekodi ya Muivory Coast-Laurent Pokou ya mabao 14 kwa kuweka rekodi mpya ya mabao 16,Misri inajivunia mastadi wake 5 katika timu bora ya Afrika Cup 2008: Kipa wao Essam al-Hadaray,beki wao mshahara Wael goma,wachezaji wake wa kiungo-Mohamed Aboutraika na Hosny Abd Rabou na bila shaka msham,bulizi aliepachika mabao 4 Amr zaky.
Makamo-bingwa kamerun wamechangia mastadi 2-mlinzi Geremi Njitap na mchezaji wake wa kiungo Alexandere Song.hata Angola imechangia alao stadi mmoja katika kikosi hicho bora cha Afrika:Mshambulizi wao manucho anaeelekea msimu huu Manchester united.
Tembo wa Ivory Coast waliopigiwa upatu sana kutoroka na kombe hili,baada ya kuteleza mbele ya Misri na halafu kupokonywa nafasi ya 3 na wenyeji Ghana hapo jumamosi, wam etoa stadi mmoja tu katika Listi hiyo:mchezaji wao wa kiungo yaya Toure.
Wenyeji Ghana kwa msangao wa wengi,imetia stadi mmoja lakini katika safu ya walinzi:mchezaji wao wa kiungo Michael Essien,aliejaza pengo la nahodha John Mensah,aliefungiwa kucheza pale Ghana ilipokutana na Kamerun katika nusu-finali.Ghana imetoa pia stadi mwengine –nae ni Sulley Muntari.
Kilichokwenda kombo na kukosolewa mno katika kombe hili la 26 la Afrika nchini Ghana ni maandalio pamoja na kasoro kadhaa zilizoonekana:
Mechi nyingi zilichezwa katika viwanja nusu-vitupu na waandazi walishindwa kuwatia shime mashabiki wa nyumbani kujaza viwanja.Au tiketi zilikua za bei ya juu ?
Kwani hata finali ya jana ilipita bila uwanja kusheheni kamili.
Viwanja -2 kati ya hivyo vikiwa vimejengwa kisasa kabisa na machina, zana nje ya viwanja hivyo hazikuridhisha.
Labda iliofedhehesha zaidi ni pale kocha wa timu mwenyeji-Ghana-mfaransa Claude Le Roy alipokosoa hadharani hali ya uwanja mkuu Accra.Alinukuliwa kusema,
„Mnamo miaka 20 ya kuwapo Afrika ,ni uwanja mbovu kabisa niliojionea.“
Kuhusu mahoteli imeonekana kwa mfano wachezaji wa bafana Bafana wakiongozwa na kocha wao mbrazil,carlos Parreira, wamezowea kupiga kambi katika hoteli za kifahari,lakini waliwekwa katika Hoteli ya daraja ya 2-star huko Tamale ambako mbuzi wakitembea bila pingamizi nje tu ya hoteli hiyo.
Halafu lile jaribio la hongo:Timu 2-Benin na namibia zilidai kwamba ziliendewa na mtu asiejulikana kuzihonga fedha ili kufanya mizengwe katika mechi zao.CAF-shirikisho la dimba la Afrika likaahidi kukichunguza kisa hicho.
Afrika kusini ikiwa ni mwenyeji wa kombe lijalo la dunia 2010 yafaa kutega sikio.Claude Leroy ametoa ushauri huu,
„Jambo la kwanza kabisa sio kuweka viti maridadi vya kupumzikia watu mashuhuri katika ukumbi wa VIP, bali ni kuona uwanja wa dimba ni safi kabisa.“