DAR ES SALAAM:Viongozi wa SADC kuijadili Zimbabwe katika kikao cha cha dharura
28 Machi 2007Wakuu wa Jumuiya na Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC wanatarajiwa kukutana mjini Dar es Salaam Tanzania hii leo, katika mkutano wa dharura kuzungumzia hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo hilo.
Suala la Zimbabwbe na hali huko Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yanatarajiwa kuwa mada kuu katika kikao hicho.
Katika wiki za hivi karibuni Zimbabwe imekuwa ikilaumiwa na jumuiya ya kimataifa kutokana na kushambuliwa kwa wanaharakati akiwemo kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Morgan Tsvangirai.
Huko Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wiki iliyopita zaidi ya watu 100 waliuawa katika mji mkuu Kinshasa, baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa kiongozi wa upinzani Jean Pierre Bemba.
Wakati huo huo Chama kinachotawala nchini Zimbabwe cha ZANU PF kimeahirisha mkutano wake mkuu uliyokuwa ujadili mpango wa Rais Robert Mugabe kusogeza mbele uchaguzi mkuu hadi mwaka 2010.
Mkutano huo ulikuwa ufanyike leo, lakini umeahirishwa kutoa nafasi kwa Rais Mugabe kuhudhuria kikao hicho cha dharura cha wakuu wa nchi za SADC.