DAR ES SALAAM : Zaidi ya watu 40 wajeruhiwa katika kampeni za uchaguzi
24 Septemba 2005Zaidi ya watu 40 wamejeruhiwa na wengine 14 kutiwa mbaroni wakati wafuasi wa vyama hasimu vya kisiasa walipopambana kaskazini mwa Tanzania kufuatia kampeni za uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa polisi na mashahidi vurugu hizo zilizuka hapo Alhamisi usiku katika mji wa kaskazini magharibi wa Bukoba kati ya wafuasi wa chama tawala CCM na wapinzani wake wakuu CUF.
Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa polisi mjini Bukoba Gregory Puka wale waliohusika walikuwa wakivurumishiana mawe na watu 14 wametiwa mbaroni kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo inasemekana kwamba ghasia hizo zilizoanzia kwa kutiana makonde zimeishia kwa kuhusisha silaha nyengine kama vile nondo na fimbo baada ya kumalizika kwa mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini humo Oktoba 30.
Hali hiyo inaonekana kuwa sio ya kawaida kwa vile uhasimu mzito wa kisiasa mara nyingi umekuwa ukiishia kwa ghasia visiwani Zanzibar ambapo hali ya mvutano imekuwa ikiongezeka na mapambano kadhaa yameripotiwa kutokea katika miezi ya hivi karibuni.
Tafauti na Zanzibar uchaguzi Tanzania Bara kwa kawaida huwa wa amani.