1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAR ES SALAAM-Rwanda kuingizwa katika Jumuia ya Afrika Mashariki ifikapo mwezi wa Novemba.

30 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CF8T

Rwanda huenda ikaingizwa katika Jumuia mpya ya Afrika Mashariki itakapofika mwezi Novemba na kufanya Jumuia hiyo kuwa na nchi nne wanachama badala ya tatu za sasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Dar es Salaam,Tanzania,baada ya viongozi wa nchi tatu za Afrika Mashariki,Rais Mwai Kibaki wa Kenya,Benjamin Mkapa wa Tanzania na Yoweri Museveni wa Uganda kumaliza mktano wao wa siku mbili,marais hao wametoa maagizo kupitia taarifa yao ya pamoja,kuwa mchakato wa kuiingiza Rwanda katika Jumuia ya Afrika Mashariki uwe umekamilika ifikapo mwezi wa Novemba.

Jumuia ya Afrika Mashariki ilizinduliwa rasmi upya mwaka 2000 ikiwa na ajenda ya kuifanya Jumuia hiyo ifanane na ya Umoja wa Ulaya,kwa kuweka ushirikiano zaidi wa kibiashara miongoni mwa raia milioni 90 wa nchi hizo tatu ili kujiimarisha zaidi kiuchumi na kisiasa.

Viongozi hao wa mataifa matatu ya Afrika Mashariki,pia wameonesha nia ya kuifanya Jumuia hiyo iwe Shirikisho la kisiasa,ambapo hatimaye nchi hizo zitakuwa na sarafu na katiba moja,itakapofika mwaka 2010 kama ilivyokubaliwa mwezi wa Agosti mwaka 2004.