1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Damu yamwagika Tahrir

3 Februari 2011

Misri haijapoa, huku watu watano wakiuawa na wengine zaidi ya 800 wakijeruhiwa katika mapambano yaliyozuka uwanja wa Tahrir, baada ya wafuasi wa Rais Hosni Mubarak kuwavamia waandamanaji wanaompinga kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/109lL
Mapambano ya mawe, fimbo na risasi
Mapambano ya mawe, fimbo na risasiPicha: picture-alliance/dpa

Usiku wa kuamkia leo, ulitanda milio ya risasi na mabomu ya petroli yaliyovurumishwa kwa waandamanaji wanaomtaka Rais Mubarak aondoke, na watu wanaoshukiwa kuwa ni wafuasi wa kiongozi huyo.

Kiasi ya wafuasi 4000 wa Mubarak waliuvamia uwanja wenye karibuni watu milioni moja, ambao kwa siku mbili sasa walikuwa wakiandamana kwa amani kudai kumalizika kwa miongo mitatu ya utawala wa Mubarak.

Maafisa wa usalama wamo?

Kijana akionesha vitambulisho vya wanachama wa Mubarak
Kijana akionesha vitambulisho vya wanachama wa MubarakPicha: Picture-Alliance/dpa

Waandamanaji waliofanikiwa kuwakamata baadhi wa washambuliaji hao, wamewaonesha waandishi wa habari vitambulisho vinavyothibitisha kuwa baadhi yao ni maafisa wa polisi na wanachama wa chama cha Mubarak.

Taarifa za kitabibu zinasema kwamba watu wanne kati ya waliouawa wana majeraha ya risasi, mmoja wao akiwa amepigwa kichwani.

Dokta Mohammed Ismail, ambaye anawapokea wahanga wa hujuma hii katika hospitali yake ya Abdulmenem Riad Square, amesema kwamba ndani ya masaa 24 yaliyopita, ameshapokea maiti saba, ingawa serikali inasema waliouawa ni watano.

Dokta Amr Bahaa, ambaye naye amekuwa akitibu majeruhi, anasema kwamba amekuwa akipokea waandamanaji waliojeruhiwa kwa risasi, ambao wanasema kuwa walifyatuliwa risasi na askari wa Mubarak ambao walivaa nguo za kiraia.

Jeshi linakanusha kufyatua risasi kwa waandamanaji na serikali pia imekataa kuwa kumekuwa na ufyatuaji wa risasi usiku wa jana.

Khaled Ghozlan, ambaye mvulana wake, Mohammed, ni miongoni mwa waliojeruhiwa kwa risasi, amesikika akimwambia kijana wake, aliyekuwa akigugumia kwa maumivu ya iodine: "Usilie mwanangu, wewe ni shujaa."

"Tumekuwapo hapa kila siku, na hatutakwenda popote. Nina watoto watano, na hata kama wote watakufa, ni sawa. Hatutaondoka hadi yeye Mubarak aondoke." Amesema Khaled.

Jeshi lalaumiwa

Mwanajeshi akijaribu kumzuia mwandamanaji asiingie uwanja wa Tahrir
Mwanajeshi akijaribu kumzuia mwandamanaji asiingie uwanja wa TahrirPicha: dapd

Jeshi la Misri linalaumiwa kwa kuyawacha matukio haya kutokea mbele ya macho yao usiku mzima, bila ya kuchukuwa hatua yoyote.

Ni kuanzia usiku wa leo tu, ndipo vifaru vinne vya jeshi vilipoanza kuelekea kwenye daraja lililopo karibu na uwanja wa Tahrir kuwafurusha wafuasi wa Mubarak, waliokuwa wakiendelea kurusha mawe kwa waandamanaji.

Hata hivyo, bado haijajuilikana, ikiwa kitendo hiki kilitokana na maamuzi rasmi ya jeshi kuingilia kati hujuma hii, au lilikuwa tukio lisilokusudiwa.

Ni waandamanaji wenyewe ndio ambao wamekuwa wakiweka vizuizi vya vyuma vizito na uzio wa mawe unaokaribia urefu wa futi 10 kuzuia wafuasi wa Mubarak wasiingie ndani ya uwanja, ambako maelfu ya wenzao wameendelea kupaza sauti za kumpinga Mubarak na kuuguza majeraha yao.

Jumuiya ya Kimataifa yalaani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: AP

Kundi la Ikhwanul-Muslimin (Udugu wa Kiislamu) ambalo ndilo kubwa nchini Misri, limemtaka Mubarak na serikali yake kuondoka madarakani mara moja.

"Tunataka utawala huu upinduliwe na tunataka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayojumuisha makundi yote." Inasema taarifa ya Ikhwanul-Muslimin iliyosomwa kwenye kituo cha televisheni cha Al-Jazeera.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekilaani kile alichokiita mashambulizi dhidi ya raia wasiokuwa na silaha, ambayo amesema hayakubaliki.

"Nina wasiwasi sana na mambo yanavyoednelea nchini Misri. Na kwa mara nyengine nazitaka pande zote zijizuie na fujo. Mashambulizi yoyote dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani hayakubaliki na nayalaani vikali." Amesema Ban Ki-moon.

Kauli kama hii imetolewa pia na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, na Ikulu ya Marekani, ambao wote wameutaka utawala wa Misri kuitisha mara moja mazungumzo na viongozi wa upinzani.

Hata hivyo, Makamo wa Rais wa Misri, Omar Suleiman, amesema kwamba hakutakuwa na mazungumzo yoyote na upinzani, hadi hapo maandamano yatakaposita.

Nao waandaaji wa maandamano nao wamesema, wanaendelea na maandamano yao na kuitisha Ijumaa ya kesho kuwa "Ijumaa ya Kuaga", wakimaanisha ndiyo siku watakayomtoa Mubarak madarakani.

Mwandishi: Martin Durm/ZPR
Mhariri: Othman Miraji