DAMASCUS-Syria yaendelea kuondoa vikosi vyake kutoka Lebanon.
31 Machi 2005Vikosi vya jeshi la Syria vimeondoka katika maeneo yake karibu na makao makuu ya jeshi na idara yake ya usalama nchini Lebanon,baada ya kuwepo vitisho vya mabomu usiku katika mji wa Beirut.
Walioshuhudia kuondoka huko kwa vikosi vya Syria,wameeleza kuwa vikosi hivyo vilibomoa maeneo yake mawili ya kijeshi karibu na Anjar,kituo muhimu cha majeshi ya Syria nchini Lebanon.
Kiasi cha malori 18 ya jeshi yaliyojaa wanajeshi pamoja na zana zao kutoka eneo hilo,karibu na kijiji cha Bonde la Bekaa,usiku kucha yalionekana yakielekea Syria.
Syria ilitoa ahadi katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan wiki hii,kuwa itamaliza kazi ya kuyaondoa majeshi yake yaliyokuwepo nchini Lebanon kwa miaka 29,kabla ya kufanyika uchaguzi wa Bunge Lebanon mwezi wa Mei mwaka huu.