1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DÜSSELDORF: Chama cha SPD kinakabiliwa na kishindo cha kushindwa

22 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFBK

Nchini Ujerumani,chama cha SPD cha Kansela Gerhard Schroeder kinakabiliwa na kishindo cha kushindwa katika uchaguzi muhimu unaofanywa hii leo katika jimbo la North Rhine Westphalia lenye wakaazi wengi kabisa.Uchaguzi huu unatazamwa kama ni kigezo kwa uchaguzi mkuu utakaofanywa mwaka ujao.Masuala ya kitaifa yametawala uchaguzi wa leo na hasa kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira uliofikia milioni 5 nchini kote na kupindukia milioni 1 katika jimbo la North Rhine Westphalia.Chama cha SPD kimetawala kwa takriban miaka 40 katika jimbo la North Rhine Westphalia, lakini uchunguzi wa maoni hivi karibuni umeonyesha kuwa SPD katika jimbo hilo,kikiongozwa na waziri mkuu wa jimbo,Peer Steinbrück kiko nyuma ya chama cha kihafidhina CDU.Katika mwaka 1999 kutoka jumla ya majimbo 16 ya Ujerumani,chama cha SPD kilitawala katika majimbo 11.Ikiwa hii leo kitashindwa katika jimbo la North Rhine Westphalia,basi SPD kitabakia na majimbo 5 tu.