1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cyprus yaomba msaada wa fedha

Josephat Nyiro Charo26 Juni 2012

Cyprus imekuwa nchi ya tano ya kanda inayotumia sarafu ya Euro kuomba msaada wa dharura wa fedha wakati ilipotangaza jana kwamba inataka fedha kuzisaidia benki zake na kuimarisha bajeti yake.

https://p.dw.com/p/15LJY
Cypriot President Dimitris Christofias makes his statement to the media at the presidential palace in divided capital Nicosia, Cyprus, Friday, June 1, 2012. Christofias said he has tasked officials to draw up plans on how the country would deal with Greece's possible exit from the eurozone. Christofias told a news conference that conditions would be 'chaotic' if debt-drowned Greece quits the euro and that the impact of such a move would be felt not only by all other countries using the currency, but all of Europe. (Foto:Petros Karadjias/AP/dapd)
Rais wa Cyprus, Dimitris ChristofiasPicha: AP

Kwa muda mrefu Cyprus ilisita kuomba msaada kwa kuwa chini ya mfuko wa kuziokoa nchi zinazokabiliwa na madeni katika kanda ya euro, msaada huja na masharti ya kubana matumizi. Serikali ya Cyprus mjini Nikosia inahofia wakopeshaji wanaweza kuilazimisha iongeze kodi inayotozwa wafanyabiashara, ambayo kitamaduni huwa chini, jambo ambalo huenda likawa kikwazo kwa wawekezaji.

Kiwango inachokihitaji Cyprus kwenye mfuko wa uokozi hakijajulikana. Waziri wa fedha wa kisiwa hicho, Vassos Shiarly, amesema nchi yake itaomba fedha za kutosha kusaidia kupunguza nakisi ya bajeti na kwamba kiwango kamili kitaamuliwa katika wiki zijazo.

Naibu waziri wa Cyprus anayehusika na uhusiano na Umoja wa Ulaya, Andreas Mavroiannis, anakadiria kutahitajika euro bilioni nne. Waziri huyo amedokeza kuwa uchumi wa nchi hiyo uko imara ingawa tatizo limetokea Ugiriki.

"Takwimu zetu kwa ujumla sio mbaya, ingawa hazikosi kasoro. Tuna shida lakini zinaweza kudhibitiwa. Tatizo linalosababisha wasiwasi ni benki za Cyprus kukabiliwa na athari za mzozo wa madeni wa Ugiriki na dhamana za Ugiriki na pia soko la Ugiriki kwa ujumla."

Bei ya hisa za kimataifa na thamani ya sarafu ya euro zimeporomoka huku wawekezaji wakibashiri kuwa viongozi wa Umoja wa Ulaya watakaokutana wiki hii kwenye mkutano wao wa kilele mjini Brusels, hawatafikia makubaliano ya njia za kuzisadiai nchi ambazo ni dhaifu kiuchumi.

Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) erläutert am Freitag (02.03.2012) auf einer Pressekonferenz in Brüssel die Ergebnisse des EU-Gipfels. Für Merkel ist die EU mit dem neuen Fiskalpakt einen wesentlichen Schritt zur Überwindung der Finanzkrise vorangekommen. Foto: Felix Kindermann   dpa
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameondoa matumaini kwamba serikali yake itaruhusu dhamana za pamoja za mikopo zitakazotolewa na kanda ya euro au hatua nyingine zinazoungwa mkono na washirika wake.

Hali ni ngumu Cyprus

Cyprus ina siku nne tu kuchanga takriban euro bilioni 1.8, ikiwa ni asilimia 10 ya pato lake jumla la kitaifa, kabla tarehe ya mwisho iliyowekewa na warekebishaji wa Ulaya kuipiga jeki benki yake ya pili kwa ukubwa, Cyprus Popular Bank, iliyoathiriwa sana na mzozo wa deni la Ugiriki.

Cyprus ingekuwa imelazimika kuomba msaada kutoka kwa mfuko wa uokozi miezi sita iliyopita, lakini wakati huo Urusi ilijitokeza kama mkopeshaji na kutoa mkopo wa euro bilioni mbili unusu wenye riba nafuu, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wake na Cyprus. Urusi huenda ikakisaidia tena kisiwa hicho. Fedha zote ilizopokea hazikutosha na sasa inalazimika kuomba msaada kutoka kwa kanda ya euro, wakati ikijiandaa kuchukua urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, Jumapili ijayo.

Hata kama Cyprus sasa inalazimika kuokolewa isifilisike kwa kutumia fedha za kigeni, naibu waziri Andreas Mavroiannis anaweka malengo makubwa kwa urais wa Cyprus wa Umoja wa Ulaya. "Wakati huu wa mzozo, watu wanaiona Ulaya kuwa sehemu ya tatizo na wala sio sehemu ya suluhisho. Tunahitaji kuubadili mtazamo huu."

Cyprus inajiunga na Ugiriki, Ireland, Ureno na Uhispania kuomba msaada wa fedha, kwa maana kwamba zaidi ya asilimia 25 ya wanachama 17 wa kanda ya euro sasa wako katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji kusaidiwa kifedha.

Mwandishi: Bormann, Thomas/Josephat Charo

Mhariri: Daniel Gakuba