1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 yasababisha ukosefu mkubwa wa ajira Marekani

9 Mei 2020

Marekani imerikodi kiwango kibaya kabisa cha kupotea kwa nafasi za ajira kutokana na athari za virusi vya corona wakati Ulaya ikiandamwa na kuongozeka kwa idadi ya vifo vinavyosababishwa na janga hilo.

https://p.dw.com/p/3bxmt
USA Las Vegas Arbeitslosigkeit
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Locher

Matumaini yamekuwa yakiongezeka kuwa kilele cha kadhia hiyo ya ulimwengu ambayo imewauwawa zaidi ya watu 270,000 kimepita  na hapo jana Marekani iliidhinisha kipimo kipya kinachoweza kutumiwa nyumbani kwa kupima mate kubaini ugonjwa wa COVID-19.

Lakini baada ya wiki kadhaa za vizuizi vikali duniani kuzuia kusambaa virusi vya corona , matokeo ya maumivu yameanza kuonekana kwa uchumi wa ulimwengu kukabiliwa na mdodoro mbaya kabisa katika kipindi cha karibu nusu karne.

Kiasi nafasi za kazi milioni 20.5 zimepotea ndani ya mwezi April huku ukosefu wa ajira ukipanda ahdi asilimia 14.7, ambacho ni kiwango cha juu zaidi tangu mdodoro wa uchumi wa miaka ya 1930.

Taifa hilo lenye uchumi mkubwa duniani limekabiliwa na kishindo cha janga la virusi vya corona ambalo tayari limesababisha vifo vya watu 75,000 nchini humo pamoja na maambukizi yanayofikia milioni 1.2

Akitilia maanani uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba, rais Donald Trump ameahidi kuifungua tena nchi hiyo na idadi kubwa ya magavana wa majimbo mbalimbali nchini Marekani wameruhusu shughuli za biashara kuanza tena japo kwa hali ya tahadhari.

Rais Trump apuuza takwimu wakati Ulaya ikichukua hatua 

USA Donald Trump in Charlotte, North Carolina
Picha: Reuters/C. Barria

Rais Trump amepuuza wasiwasi unaotokana na takwimu hizo akisema ishara za hivi karibuni za kuimarika kwa masoko ya mitaji ni uthibitisho kuwa mambo yatatengamaa katika kipindi kifupi kinachokuja.

"Tutakuwa na mwaka mzuri, hapo mwakani na nadhani utatujia kama upepo " amesema Trump wakati wa mkutano wake na waandishi habari mjini Washington.

Matumaini yake yanakuja wakati virusi vya corona vikiripotiwa kusambaa ndani ya ikulu ya White House baada ya msemaji wa makamu wa rais Mike Pence kugundulika kuwa ameambukizwa.

Katika taifa jirani la Canada, kiasi nafasi za kazi milioni 3 zimepotea na kusababisha kiwango cha ukosefu wa ajira kupanda hadi asilimia 13.1 , siku mbili tangu Umoja wa Ulaya ulipobashiri kutokea mdodoro mkubwa wa uchumi kwenye kanda hiyo.

Katika hatua nyingine mawaziri wa Fedha wa mataifa ya kanda ya sarafu ya Euro wameidhinisha kiasi dola bilioni 260 kuyasaidia mataifa ya Ulaya kufidia gharama kubwa za kupambana na mlipuko wa virusi vya corona.

Mpango huo utaosimamiwa na mfuko wa uokozi wa kanda ya sarafu ya Euro ni hatua kubwa ya kwanza katika juhudi za Umoja wa Ulaya kuupiga jeki uchumi ambao makadirio yanaonesha utasinyaa kwa asilimia 7.7 mwaka 2020.

Chini ya makubaliano hayo kila nchi mwanachama wa umoja wa sarafu ya Euro itaweza kuchukua mkopo wa riba nafuu huku mataifa yaliyoathriwa zaidi kama Italia na Uhispania yatapatiwa kiwango kikubwa cha fedha za uokozi.

Dawa ya Madagascar yawasili Tanzania

Madagaskar Antananarivo | Coronakrise | angeblich heilender Tee
Picha: Getty Images/AFP/Rijasolo

Katika hatua nyingine Umoja wa Ulaya pia umetangaza kufikiwa makubaliano ya kurefusha muda wa kuifunga mipaka na mataifa mengine hadi Juni 15 ili kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.

Kwengineko Tanzania jana imepokea shehena ya kwanza ya dawa ya mitishamba ambayo serikali ya Madagascar imedai mara kadhaa kuwa inatibu ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vy corona.

Hayo yamethibitshwa na msemaji wa serikali ya Tanzania, Hassan Abbas aliyeandika kupitia ukurasa wa Twitter kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki imepokea msaada wa dawa hiyo kutoka Madagascar.

Mataifa kadhaa ya Afrika tayari yameelezea nia ya kuagiza shehena za dawa hiyo iitwayo Covid-Organics kutoka Madagascar  ambayo imetengezwa kwa mmea wa Artemisia unaopatikana kwa wingi katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi.

Hata hivyo shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO limeonya jana dhidi ya kutumiwa dawa hiyo ambayo bado haijafanyiwa utafiti wa kutosha kuthibitisha uwezo wake wa kutibu COVID-19