Covid-19: Tanzania yanza kutoa elimu kwa njia ya TV, redio
21 Aprili 2020Wizara ya elimu sayansi na teknolojia inaamini kuwa mfumo huo mpya utawawezesha wanafunzi wanaoendelea kusalia majumbani kupata elimu na kuanza kuwaandaa wanafunzi wa kidato cha sita, nne na wale wa darasa la saba na pili wanaokabiliwa na mitihani baadaye mwaka huu.
Taasisi ya elimu Tanzania ndiyo inayoratibu na kuandaa masomo hayo ikishirikiana na vituo vya televisheni na redio. Mbali ya televisheni mbili zinazorusha masomo hayo, kadhalika redio 34 za kijamii zimekubali kushiriki kwenye mpango huo zikipeperusha masomo hayo kote nchini.
Katibu mkuu wa wizara ya elimu, sayansi ya teknolojia Dr Leonard Akwilapo amesema mpango huo una shabaha ya kuwezesha wanafunzi kurudia baadhi ya masomo waliyokwisha yapitia wakati wakiwa shuleni na pia kupata masomo mapya.
Wakati huu wanafunzi wameendelea kusalia majumbani ingawa baadhi yao wamekuwa wakiendelea na masomo kwa njia ya mitandao.
Wakati ikiwa haijulikani ni lini shule hizo zitakapofunguliwa tena, Wizara inasema urushwaji wa vipindi hivyo siyo kwamba ni mbadala wa masomo ya darasani wakati masomo katika shule hizo yatakaporejea katika hali yake ya kawaida.
Visa vya maambukizi vyazidi kupanda
Katika hatua nyingine, Tanzania imeendelea kurekodi kiwango cha juu cha maambukizi ya virusi vya corona na hadi Jumatatu jioni, idadi ya waliogundulika kuambukizwa ilifikia 254.Takwimu zinaonyesha kwamba watu waliopoteza maisha tangu janga hilo liingie nchini ni 10, huku Dar es salaam na Zanzibar ikiwa ndiyo yenye maambukizi zaidi.
Wakati juhudi za kutoa elimu kukabiliana ugonjwa wa covid-19 zikiendelea wizara ya afya imeandaa maombi maalumu kwa taifa yatayofanyika kesho katika viwanja vya Karemjee. Maombi hayo ambayo yatahudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yatawaleta pamoja pia viongozi mbalimbali wa madhehebu ya kidini.
Wakati huo huo, chama cha wanasheria Tanzania bara cha Tanganyika Law Society Jumanne kimesambaza waraka wake kikipendekeza mambo kadhaa ya kuzingatiwa ili kukabiliana na maambukizi ya janga hilo.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuitaka serikali kuhakikisha vifaa vya kujikinga na maambukizi hayo vinasambazwa na kutolewa bure kwa wananchi, kuweka marufuku ya mikusanyiko ya watu katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenye baa, sherehe za harusi na mikutano ya viongozi wa serikali.