1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 ni kitisho kwa waliopoteza makaazi

Admin.WagnerD28 Aprili 2020

Mamilioni ya watu waliolazimika kuyahama makaazi yao kutokana na mafuriko, vimbunga na vita sasa wanakabiliwa na hatari ya kuzongwa na janga la virusi vya corona. Hayo ni kulingana na ripoti mpya iliyochapishwa leo.

https://p.dw.com/p/3bVKu
Syrien Flüchtlingskonvoi bei Sarmada in der Provinz Idlib
Picha: Reuters/K. Ashawi

Ripoti hiyo iliyotolewa na kituo cha kimataifa kinachofuatilia watu wanaoyakimbia maskani yao, IDMC, imesema mwaka 2019 hali mbaya ya hewa iliwalazimisha kiasi watu milioni 24 kote duniani kuhama kutoka maeneo waliyokuwa wakiishi.

Watu wengine karibu milioni 9.5 walilazimika kuchukua hatua kama hiyo kutokana na masuala mengine, vikiwemo vita.

Mamilioni ya watu walikimbia mafuriko, vimbunga, moto wa nyika, ukame, maporomoko ya udongo, matetemeko ya ardhi na hali mbaya ya hewa kama joto lililopindukia viwango vya wastani.

Kulingana na ripoti ya IDMC, karibu watu milioni 51 wamepoteza makaazi na wengi wanaishi kwenye kambi zenye mifumo dhaifu ya usafi na sasa wanazongwa na kadhia ya janga la virusi vya corona.

Hali duni ya afya ni changamoto kubwa

Unruhen in Mali 2019 | Flüchtlingscamp
Picha: Getty Images/AFP/M. Cattani

Ripoti hiyo imeorodhesha masuala kama ukosefu wa maji, sabuni na vifaa vingine vya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kuwa kitisho cha wazi katika makambi au makaazi duni yanayohifadhi watu hivi sasa.

Kadhalika vizuizi na marufuku chungu nzima zilizowekwa duniani kukabiliana na virusi vya corona zimefanya kuwa vigumu kwa maeneo kama shule, kumbi za makanisa au hata viwanja vya wazi kutoa maeneo ya muda kuwahifadhi watu waliopoteza makaazi.

Serikali pia haziwezi tena kujaza magari na kuwahamisha watu kwa wingi kutoka maeneo yaliyo kwenye hatari.

Na juu ya hilo watu wasio na makaazi hawana uwezo wa kifedha wala uhakika wa hifadhi ya chakula katika wakati mgumu kama sasa unawalazimisha kubakia sehemu moja kuepuka maambukizi.

Kwa ujumla ripoti ya IDMC inaonya kuwa hamkani si shwari, na mfululizo wa majanga unawatia kishindo wote waliopoteza makaazi.

Mabadiliko ya Tabianchi yanachochea mzozo 

Nigeria Trinkwasser-Brunnen
Picha: Getty Images/AFP/L. Tato

Kwenye mataifa kama Nigeria, Sudan Kusini na Yemen, mamia kwa maelfu ya watu kwanza walilazimishwa kuyahama maeneo yao kutokana na vurugu na kisha baadaye majanga ya ukame na mafuriko.

Nchini Burkina Faso, Mali na Niger wengi wamepoteza makaazi kutokana na ukosefu wa maji na mapigano yanayoendelea.

Na juu ya yote hayo, sasa wanazongwa na hofu ya janga la kiafya la virusi vya corona.

Pamoja na hayo, ripoti hiyo ya IDMC imegusia pia jinsi mabadiliko ya tabia nchi yanavyochochea hali kuwa mbaya duniani na kuwasukuma watu kukimbia kutoka maeneo yao ya asili.

Viwango vya joto vinavyoongezeka nchini Marekani na Australia vilichochea moto wa nyika mwaka uliopita na mwanzoni mwa mwaka 2020.

Joto pia linapanda baharini na kuleta vimbunga vya kila wakati.

Ripoti ya IDMC imezirai serikali duniani kuwa macho kwa sababu pindi maeneo mengi yanayohifadhi watu wasio na makaazi yatavamiwa na kadhia ya virusi vya corona, athari itakuwa kubwa zaidi kuliko mashaka yaliyosababishwa na majanga mengine.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Mohammed Khelef