1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cote d'Ivoire yamtema Drogba

22 Machi 2013

Cote d'Ivoire imemtema nyota Didier Drogba wakati ikielekeza macho yake katika dimba la kombe la dunia la mwaka wa 2014 nchini Brazil.

https://p.dw.com/p/182lw
RUSTENBURG, SOUTH AFRICA - JANUARY 26, Yaya Toure (M) of Ivory Coast celebrates scoring a goal with Didier Drogba and Max Gradel during the 2013 African Cup of Nations match between Ivory Coast and Tunisia at Royal Bafokeng Stadium on January 26, 2013 in Rustenburg, South Africa. (Photo by Lefty Shivambu / Gallo Images/Getty Images)
Fußball 2013 African Cup of Nations - Elfenbeinküste gegen TunesienPicha: Getty Images

Mabingwa wapya wa Afrika Nigeria pia wamerejelea harakati za kufuzu kwa dimba hilo wikendi hii bila huduma za mshambuliaji wake aliyejeruhiwa Emmanuel Emenike. Miongoni mwa mechi 20 za kufuzu katika kombe la dunia, zinazochezwa barani Afrika ni pamoja na Cote d'Ivoire dhidi ya Gambia, Nigeria inawaalika Kenya nao maafisa wa Misri kwa mara ya kwanza wamewakubalia mashabiki kuingia uwanjani kutazama mchuano wao dhidi ya Zimbabwe. Cote d'Ivoire, Nigeria na Misri zinaongoza makundi yao ya kufuzu katika juhudi za kujipa moja kati ya nafasi tano zilizotengewa bara Afrika katika dimba la dunia.

Kocha wa Cote d'Ivoire Sabri Lamouchi amesema amemwacha nje mshambuliaji wa Galatasaray Didier Drogba kwa sababu ya hofu ya hali yake ya sasa, lakini akapuuzilia mbali wasiwasi kuwa huo huenda ukawa mwisho wa barabara ya kimataifa ya mshambuliaji huyo mshindi wa Premier League na Champions League.

Didier Drogba amewasaidia Galatasaray wa Uturuki kufuzu katika robo fainali ya Champions League
Didier Drogba amewasaidia Galatasaray wa Uturuki kufuzu katika robo fainali ya Champions LeaguePicha: Reuters

Hata ingawa Cote d'Ivoire wanapigiwa upatu kuwashinda Gambia leo Jumamosi na hata kufuzu katika kombe la dunia, huenda Drogba asiweze kushinda taji lolote kuu la kimataifa akiwa na kikosi cha taifa. Atakuwa takribani na umri wa miaka 37 wakati wa dimba lijalo la kombe la mataifa ya Afrika AFCON. The Super Eagles wa Nigeria inachuwana leo na Harambee Stars wa Kenya mjini Calabar. Vijana hao wa kocha Stephen Keshi wanatarajiwa kuongoza kundi F mbele ya Namibia, Malawi na Kenya.

Misri haikufuzu katika dimba la AFCON mwaka wa 2012 na 2013 baada ya wimbi la machafuko ya kisiasa kusambaa hadi uwanjani wakati zaidi ya watu 70 waliuawa katika mchuano wa ligi mjini Port Said mwaka mmoja uliopita, mkasa ambao bado unaiumiza kandanda ya Misri. Leo takribani mashabiki 30,000 wameruhusiwa kutazama mechi yao dhidi ya Zimbabwe katika uwanja wa Alexandria licha ya malalamiko ya awali ya Zimbabwe kuwa mchuano huo uchezwe katika nchi nyingine.

Cameroon inamenyana na Togo mjini Yaounde wakati Samuel Eto'o na Emmanuel Adebayor wakichukua usukani wa timu zao, lakini timu zote zinapambana kufuzu katika kundi lao zikiwa nyuma ya Libya na Congo katika kundi I. Cameroon imekosa vinyang'anyiro viwili vilivyopita vya AFCON na siyo tena mwamba wa soka barani Afrika, na ijapokuwa Togo iliridhisha kwa kufika robo fainali, haijashinda katika mechi mbili za kufuzu katika kombe la dunia. Senegal wanachuana na Angola nchini Guinea kutokana na adhabu ya kupigwa marufuku ya mwaka mmoja uwanja wa Leopold Senghor baada ya vurugu zilizozuka katika mchuano wa kufuzu dimba la AFCON mwezi Oktoba mwaka jana. Ghana, timu nyingine inayoumia kutokana na uchungu w akutoshinda dimba la AFCON, inawaalika Sudan katika kundi D linaloongozwa na Zambia.

Mshabuliaji wa Cameroon Samuel Eto'o kwa sasa anachezea klabu ya Urusi ya Anschi Machatschkala
Mshabuliaji wa Cameroon Samuel Eto'o kwa sasa anachezea klabu ya Urusi ya Anschi MachatschkalaPicha: Reuters

Katika mechi za kesho Jumapili, Tanzania wanawaalika wageni Morocco katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Viongozi wa kundi B Tunisia wanapamba na nambari mbili Sierra Leone, Algeria dhidi ya Benini Jumanne ijayo. Mali watapambana na Rwanda wakati Ethiopia ambao wanaogoza kundi A wakipambana na Botswana kesho Jumapili. Afrika Kusini wanahitaji kuwazaba Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Cape Town.

Kevin-Prince Boateng akutana na Blatter
Kiungo wa klabu ya AC Milan Kevin Prince Boateng ambaye aliwaongoza wachezaji wenzake kuondoka uwanjani mwezi Januari baada ya kubaguliwa kwa msingi ya rangi, anaamini kuwa mchezo wa kandanda unastahili kuwa na tamaduni mbalimbali.

Mchezaji huyo wa Ghana amesema kuwa kitendo hicho chake wakati wa mchuano dhidi ya klabu ya daraja la nne Pro Patria hakikuwa kizuri, lakini amesema kuwa mabadiliko muhimu yanahitaji katika soka. Boateng amekutana jana Ijumaa na Rais wa Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA Sepp Blatter ambapo wamejadili kuhusu suala la ubaguzi wa rangi katika kandanda. Mchezaji huyo Mghana anasema anatumai kuwa karibuni kutakuwa na Jose Mourinho mweusi, au Pep Guardiola Mpakistani katika kandanda, akiongeza kuwa inafaa pawepo adhabu kali kwa watu na vilabu vinavyopatikana na hatia ya kufanya ubaguzi wa rangi.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/Reuters/AFP

Mhariri Yusuf Saumu