Corona: Wahudumu wa maabara Kenya watishia kugoma
29 Desemba 2020Sekta ya afya nchini Kenya inakabiliwa na msukusuko kutokana na mfululizo wa migomo ya wahudumu wa afya katikati ya janga la virusi vya corona.
Muungano wa wahudumu wa maabara nchini Kenya umetoa muda wa hadi Januari 4 mwaka unaokuja kwa serikali kushughulikia madai yao au wajiunge na wauguzi na maafisa wa kliniki walio kwenye mgomo kwa muda wa siku 25 hivi sasa.
Kupitia muungano wao, KNUMLO, wahudumu hao wameisuta serikali wakisema imepuuza kitengo hicho muhimu huku juhudi zao, kushirikisha mazungumzo na asasi za serikali zikigonga mwamba kama anavyoelezea katibu mkuu Chrispine Momanyi.
"Endapo siku saba kuanzia sasa, taifa lote, iwe hata ni sekta ya binafsi, shirika la umma kama CDC, tunashirikiana kusitisha huduma zozote kwa hii serikali na wananchi kwa sababu hatuchukuliwi kuwa watu muhimu."
Kiasi wahudumu wa maabara 267 wameambukizwa virusi vya Corona
Mwenyekiti wa muungano wa wahudumu hao Adel Ottoman anasema wahudumu wa maabara wanakabiliwa na hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya korona akieleza kuwa, kati ya idadi jumla ya wahudumu wote wa afya nchini waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid 19 asilimia 85 ni wahudumu wa maabara hii ikiwa ni wahudumu 50.
Ottoman, ameongeza kuwa, wahudumu wa maabara 267 wameambukizwa virusi vya homa kali ya korona hii ikiwa ni kuanzia mwezi Machi wakati janga la korona liliporipotiwa kwa mara ya kwanza nchini. Miongoni mwa matakwa yao wakishinikiza kuajiriwa kwa wahudumu zaidi 7,000 na wahudumu waliokwenye mikataba kuajiriwa kikamilifu.
"Tunataka wahudumu wa maabara kualikwa kwa mazungumzo, hatuelewi ni vipi utaalika mtu ambaye hata hawezi kudhibitisha endapo mtu yupo na virusi vya korona."
Wahudumu hawa sawia na wenzao, wanashinikiza serikali kuhakikisha wanapata mavazi maalum ya kuwakinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya korona PPEs pamoja na kuongezewa marupurupu kufikia shilingi elfu 30 za Kenya kwa kuhatarisha maisha wakiwa kazini.
Mfululizo wa migomo ya watumishi wa sekta ya afya nchini Kenya, kwa sehemu kubwa imewaacha wananchi njiapanda, wengi wakiishia kutafuta huduma za matibabu kwenye hospitali binafsi ambako, gharama ya matibabu ni ghali ikilinganishwa na hudumu katika hospitali na vituo ya afya vya umma.
Licha ya serikali ya Kenya kufanikisha kumaliza mgomo wa madaktari hivi karibuni kwa kufikia makubaliano ya kumaliza matatizo yanayowakabili, ni dhahiri mgomo unaondelea wa maafisa wa kiliniki na kitisho cha mgomo mpya kutoka kwa wahudumu wa maabara vitaathiri huduma kwa umma.