1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona mada kuu Mkutano wa Kilele Ulaya

25 Machi 2021

Rais wa Marekani Joe Biden atajiunga kwa njia ya video na viongozi wengine katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya. Kuna mengi yatakayojadiliwa ila mada kuu katika mkutano huo itasalia kuwa janga la virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3r6bm
EU-Gipfel Covid-19
Picha: Olivier Hoslet/AP Photo/picture alliance

Mgeni wa heshima katika mkutano huu wa kilele utakaofanyika kwa njia ya video atakuwa mtu ambaye wanasiasa wengi wa Umoja wa Ulaya walikuwa wakimfahamu kama mtu aliyekuwa katika nafasi ya pili nyuma ya rais wa zamani Barack Obama.

Lakini sasa Joe Biden ambaye mwenyewe anakishikilia kitihicho cha urais, atajiunga na mkutano huo mwendo wa saa 8.45 usiku moja kwa moja kutoka Washington kwa ajili ya mazungumzo yatakayojikita katika ushirikiano wa kimataifa na Umoja wa Ulaya na pia kuyapunguza makali ya Urusi na China.

USA Amoklauf in Boulder Colorado | Joe Biden
Rais Joe Biden wa MarekaniPicha: Mandel Ngan/AFP

Ni fahari kubwa kuona uhusiano wa Transatlantic ukifufuliwa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajia Rais Biden hatoliibua suala la mradi wa usafirishaji gesi kutoka Urusi hadi Ulaya maarufu kama Nord Stream 2. Biden kama mtangulizi wake Donald Trump anaupinga mradi huo ila Merkel anauunga mkono licha ya ukosoaji kutoka kwa baadhi ya nchi za Ulaya pia. Kuelekea mkutano huo wa kilele, wabunge wa Ujerumani wanasema hakuwezi kuzuka mzozo kuhusiana na mradi huo.

Umoja wa Ulaya unasema ni fahari kubwa kuona uhusiano wa transatlantic unafufuliwa tena. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken tayari alifanya mazungumzo na rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Urusula von der Leyen mjini Brussels jana. Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye alikuwa anauponda Umoja wa Ulaya, hakuwahi kualika kwenye mkutano huo wa kilele lakini watangulizi wake Barack Obama na George W. Bush walikuwa wanapata mialiko.

Joe Biden hajapangiwa kuzungumza kwa muda mrefu ila labda watakaohudhuria mkutano huo watamuuliza iwapo kuna uwezekano wa Marekani kuzisaidia nchi za Umoja wa Ulaya na chanjo. Ugavi wa chanjo ni suala nyeti mno la kujadiliwa kwa njia ya video katika mkutano huo wa kilele, ukizingatia kwamba idadi ya maambukizi ya virusi vya corona inazidi kuongezeka kote barani Ulaya.

Weltspiegel | 25.03.2021 | Bilder des Tages | Tableau
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Marekani ambayo kufikia sasa haijasafirisha chanjo zozote nje ya nchi yake, inakadiria kwamba mwishoni mwa mwezi Mei itakuwa imekamilisha kuwachoma chanjo raia wake. Baada ya hapo kutakuwa na uwezekano wa kupelekea nchi zengine chanjo hizo.

Umoja wa Ulaya wataka kuboresha uhusiano na Uturuki

Ongezeko la maambukizi lililochangiwa na aina mpya ya virusi vya corona, limezipelekea nchi za Umoja wa Ulaya kuzungumzia mno suala la chanjo. Tangazo lililowashangaza wengi ni lile lilotolewa na Kansela Angela Merkel la kuondoa vikwazo vya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona wakati wa likizo ya Pasaka kwani Ubelgiji na Ufaransa wameweka vikwazo vipya katika kipindi hicho hicho.

Mbali na virusi vya corona, mada nyengine itakayozungumziwa katika mkutano huo ni Uturuki. Umoja wa Ulaya unataka kuuboresha uhusiano wake na Uturuki licha ya kuwa kumeshuhudiwa vitendo vya uchokozi kutoka kwa nchi hiyo. Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya amesema kwamba kwa sasa mzozo ulioko mashariki mwa bahari ya Mediterenia ambapo Uturuki inazozana na Cyprus na Ugiriki kuhusiana na uchimbaji gesi umetulia kidogo. 

 LINK: http://www.dw.com/a-56978504