Wagonjwa wanaokutikana na kirusi kipya cha Delta waongezeka
29 Juni 2021Waziri wa afya wa Ufaransa Olivier Veran amesema kuwa asilimia 20 ya wagonjwa wa Covid-19 nchini Ufaransa wamekutikana na kirusi kipya cha Corona aina ya Delta. Wakati huo huo, utafiti uliofanywa nchini Uingereza umeonyesha kuwa kuchanganya dozi mbili tofauti za chanjo kunaimarisha kwa kiwango kikubwa kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.
Waziri wa afya wa Ufaransa Olivier Veran amesema kirusi kipya aina ya Delta kinaendelea kusambaa duniani kote japo pole pole. Kirusi hicho ambacho kiligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini India, kinatajwa kuwa hatari kwani kinaambukiza kwa kasi zaidi.
"Aina mpya ya kirusi cha Corona-Delta kimechangia karibu asilimia 20 ya wagonjwa wapya wa Covid-19. Na idadi ya wagonjwa waliokutikana na aina hiyo ya kirusi inazidi kuongezeka japo maambukizo kwa ujumla yanapungua."
Soma zaidi: Afrika yakabiliwa na wimbi la 3 la corona
Wagonjwa wapya 509 waliambukizwa ugonjwa huo jana Jumatatu nchini Ufaransa japo kiwango cha maambukizo mapya katika muda wa siku saba kimepungua hadi 1,819. Idadi hiyo ikiwa ndogo zaidi kurekodiwa katika muda wa miezi kumi, tofauti na kilele cha maambukizo mnamo mwezi Aprili ambapo wakati huo kuliripotiwa wagonjwa 42,225.
Jana Jumatatu, Ujerumani ilisema maambukizo mapya yanayoripotiwa nchini na ambayo yamesababishwa na aina mpya ya kirusi cha Corona yameongezeka mara mbili zaidi katika muda wa wiki moja. Hatua hiyo imesababisha baadhi ya nchi kuweka tena vizuizi vya usafiri.
Wakati hayo yakiarifiwa, utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza umeonyesha kuwa kucheleweshwa kwa dozi ya pili na tatu ya chanjo ya AstraZeneca kunaimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.
Utafiti huo umeonyesha kuwa kucheleweshwa kwa muda kati ya chanjo ya kwanza na pili kwa hadi wiki 45 kunaimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, kinyume na hofu ya awali kuwa kuchelewesha muda wa chanjo baina ya dozi ya kwanza na ya pili kunaathiri kinga.
Mkuu wa utafiti katika chuo kikuu cha Oxford Andrew Pollard amesema kuwa, kuchanjwa dozi ya tatu zaidi ya miezi sita baada ya mtu kupokea chanjo ya pili pia kunaimarisha zaidi kinga dhidi ya ugonjwa huo unaoshambulia zaidi mapafu.
Vile vile, utafiti tofauti uliotolewa jana Jumatatu ulionyesha kuwa kuchanganya dozi ya AstraZeneca na ile ya Pfizer/BioNTech pia kunaimarisha kinga zaidi dhidi ya Covid-19.
Mathew Snape, mkuu wa utafiti wa majaribio ya chanjo, amesema wakati aina mbili za chanjo zinapochanganywa na kutolewa kwa mtu katika muda wa wiki nne, basi mwili wa mtu unajenga kinga imara dhidi ya Covid-19.
Na nchini China, wizara ya afya imetoa ripoti iliyoonyesha kuwa nchi hiyo ya Mashariki mwa Asia imewachanja zaidi ya watu milioni 20.9 jana Jumatatu na kufikisha idadi jumla ya watu waliochomwa chanjo dhidi ya Covid-19 nchini humo kuwa watu bilioni 1.2.