1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Copa America -Brazil ni mabingwa tena

16 Julai 2007

Brazil imerudi na Copa America nyumbani Rio baada ya kuilaza jana Argentina kwa mabao 3:0.Mexico imetokea 3.

https://p.dw.com/p/CHbh

Mabingwa wapya na wa zamani wa Copa America ni Brazil walioizaba Argentina jana mabao 3:0.

Katika kombe la dunia la vijana huko kanada, Chile imeipiga kumbo Nigeria kwa mabao 4:0.Tutawachukua katika All-Africa Games-michezo ya bara la Afrika mjini Algiers kusikia jinsi wanariadha wa Kenya na Tanzania walivyotamba au la.

Katika finali ya jana ya kusisimua ya Copa America-mabingwa Brazil waliichezesha Argentina-kindumbwendumbwe na kuizaba mabao 3:0 na kurudi na kombe Rio de Jeneiro kwa mara ya pili mfululizo.licha ya kuambiwa hwana lao jambo mara hii walipolazwa mabao 2:0 na Mexico iliomaliza nafasi ya tatu,Brazil iliistusha Argentina kwa bao la haraka mnamo dakika ya 4 ya mchezo pale Julio Baptista alipolifumania lango la Argentina.

Wakiwa wamefadhahika –nahodha wa Argentina Roberto Ayala,akiichezea Argentina mara yake ya 115,alitia bao katika lango lake mwenyewe wakati akijaribu kuokoa.Kabla kipindi cha mapumziko Brazil ikitamba kwa mabao 2:0.

Msumari wa mwisho katika jeneza la Argentina kwenye Copa America 2007,ulipigwa na Daniel Alves.Stadi wa Argenetina Juan Roman Riquelme alitiwa mfukoni na hakuonekana kati ya uwanja.

Pigo la jana ni kali sana kwa Argentina iliolazwa finali kama hii miaka 4 nyuma kupitia mikwaju ya penalty.

Kocha mpya wa Brazil Dunga, amesherehekea ushindi wake wa kwanza tangu kushika hatamu za timu hii kufuatia Kombe la dunia nchini Ujerumani.

Kwani hilo limekuwa pigo la 3 mfululizo dhidi ya Brazil:Utakumbuka kuwa Brazil iliikumta Argentina mabao 4:1 katika Confederations Cup hapa Ujerumani 2005 na halafu ikailaza kwa mabao 3:0 katika mchezo wa kirafiki mwaka jana.

Copa America 2007 ndilo lililojionea mabao mengi kabisa katika historia ya Kombe hili-mabao 86 yametiwa hadi jana-hii ikiwa rekodi.Copa America lilianiwa na mabingwa Brazil,makamo-bingwa Argentina,wenyeji Venezuela,Colombia,Ecuador,Paraguay,Peru na Uruguay lakini pia timu za Amerika ya kaskazini-kama Marekani na Mexico kutoka Amerika ya kati.

Copa Amerika lilianzishwa hata kabla ya kombe la dunia-ilikua 1916 na kama katika kombe la dunia, washindi wa kwanza walikua Uruguay.Mara ya mwisho Uruguay kuvaa taji 1995.

Mabingwa wa Ujerumani –Bundesliga-Stuttgart waliarifu jana kwamba wanamuajiri mbrazil Ewerthon kutoka Real zaragoza, akiwa mbrazil 3 kujiunga na Bundesliga mnamo siku 3.Ewerthon alikwishacheza katka Bundesliga 2001 hadi 2005 alipichezea Borussia Dortmund.

Juzi,mbrazil mwengine Ailton alijiunga na Duisburg,inayopanda daraja ya kwanza baada ya kuichezea hapo kabla Bremen na baadae Schalke .Carlos Alberto mbrazil mwengine anahamia werder Bremen.

Katika kombe la dunia la chipukizi chini ya umri wa miaka 20,Chile imeipiga kumbo Nigeria mabao 4:0 na sasa ni wao wanaocheza na Argentina katika nusu-finali.Argentina iliitoa Mexico kwa bao 1:0.Mabao yote 4 ya Chile yalitiwa baada ya mchezo kurefushwa.Katika nusu-finali ya pili hapo jumatano, Argentina ina miadi na Chile.Austria itacheza nusu-finali ya kwanza hapo jumatano na Jamhuri ya Czech.

Mashindano ya ubingwa wa riadha ulimwenguni yakikaribia huko Osaka,Japan,mwezi ujao, jogoo la Ethiopia Kenenisa Bekele limeanza kuwika na kuwatahadharisha wale wote ambao waliota ndoto ya kumuangusha:

Katika changamoto yam bio za mita 3000 huko Shefield,Uingereza,hapo jana bingwa huyo wa olimpik na dunia wa mita 10.000 alinyakua ushindi kwa muda wake wa dakika 7 na sek.26.69 rekodi ya mashindano hayo ya Grand Prix.

ALL-AFRICA GAMES:

Katika michezo ya bara la Afrika-All-Africa Games huko Algiers, Algeria,Bafana Bafana au Afrika kusini ina miadi leo na samba wa nyika-Kamerun huko Boumerdes wakati zambia inakabiliana na Algeria-wenyeji mjini Kolea.Kuna pia leo mashindano ya Vollyball na basketball huko Blida na Algeris.

Katika michezo ya walemavu, Kenya imetamba kwa medali 6 za dhahabu hadi sasa.Abraham Tarbei alitamba katika mita 5000 na hii ikaifanya Kenya kukusanya tayari hadi jana medali 6 za dhahabu.