1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Viongozi wasema wakati wa kuyaokoa mazingira ni sasa

Caro Robi
15 Novemba 2017

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesisitiza kuwa nchi zilizoendelea zina wajibu mkubwa wa kuyalinda mazingira ikilinganishwa na nchi zinazoendelea na nchi ndogo za visiwani.

https://p.dw.com/p/2ngrG
UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Espinosa & Macron Bainimarama & Merkel & Guterres
Picha: Reuters/W. Rattay

Rais Steinmeier amesema nchi zinazoendelea na za visiwani zinachangia kwa kiasi kidogo mno katika uchafuzi wa mazingira yanayosababisha mabadiliko ya tabia nchi lakini ndizo zinazoathirika pakubwa na kuwa katika hatari ya kuangamia kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kama vimbunga, mafuriko, joto la kupita kiasi na kina cha maji ya bahari kuongezeka ilhali sauti zao hazijapewa nafasi kubwa ya kusikika ulimwenguni.

Steinmeier ameongeza kusema kuwa makubaliano ya kuyaokoa mazingira yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa, mwaka 2015 yatakuwa tu ya ufanisi iwapo yatatekelezwa kikamilifu huku akiyasifu mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea hapa Bonn kwa siku kumi zilizopita kama ya tija.

Viongozi kuongoza juhudi za kuyalinda mazingira

Rais huyo wa Ujerumani anawaongoza viongozi wengine takriban 30 wa nchi mbali mbali katika mkutano huo wa kimataifa wa mazingira hapa Bonn. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambao wametwishwa jukumu la kuwa manahodha wa kuuongoza ulimwengu kufikia malengo ya kuyaokoa mazingira watahutubia pia leo katika mkutano huu wa COP23.

UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Steinmeier & Macron
Rais wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier na wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/W. Rattay

Wanaharakati wa kuyalinda mazingira wanamtaka Merkel kuwa katika mstari wa mbele kuchukua hatua madhubuti za kupunguza kiwango cha gesi chafu ya Carbon inayotoka viwandani ambayo ni mojawapo ya vichocheo vya kuongezeka kwa joto duniani.

Ujerumani bado inazalisha kwa wingi nishati ya makaa ya mawe ambayo inachangia asilimia 40 ya umeme nchini humu na inahofiwa huenda nchi hii ikashindwa kufikia malengo yake ya kupunguza kwa asilimia 40 gesi chafu ya Carbon ifikapo mwaka 2020.

Je Ujerumani itafikia malengo yake?

Makundi ya watetezi wa mazingira yamefanya maandamano nje ya ukumbi wa mkutano wa COP23 kupinga matumizi ya makaa ya mawe Ujerumani. Ni wakati mgumu kwa Merkel ambaye anajaribu kuunda serikali ya mseto na vyama vya kijani cha walinda mazingira na cha Free Democrats FDP ambapo mojawapo ya masuala makuu yanayozua utata ni la mazingira.

Kampuni za kuzalisha nishati zimeonya kuwa nishati ya makaa ya mawe inahitajika kuhakikisha kuwa kuna kiwango cha kutosha cha nishati ya kuendesha viwanda Ujerumani, taifa imara zaidi kiuchumi barani Ulaya.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuendelea kuwekeza katika nishati za makaa ya mawe, mafuta na gesi kutasababisha kuangamia kwa binadamu katika siku za usoni akizitaka nchi kutowekeza kifedha katika nishati hizo zenye madhara kwa mazingira.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Ap

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman