1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Uwekezaji zaidi uelekezwe kwa sekta ya kilimo

Caro Robi
10 Novemba 2017

Kuwekeza haraka na zaidi katika suala la kilimo na kuwasaidia wakulima wadogo, kutasiaidia pakubwa katika kupunguza kutolewa kwa gesi chafu na kuwalinda watu dhidi ya athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/2nQWZ
Bangladesch   Jhum Kultur
Picha: DW/M. Mamun

Hayo yalisemwa katika mkutano wa kimataifa wa mazingira unaofanyika mjini Bonn, Ujerumani tangu Jumatatu tarehe sita. Waziri wa chakula na kilimo wa Ujerumani Christian Schmidt amesema kilimo ni nyanja muhimu ya kujipatia riziki hasa katika maeneo ya vijijini na inachangia pakubwa katika kuhakikisha kuna chakula cha kutosha huku wakati huo huo, iwapo kilimo kitashughulikiwa vizuri kinaweza kuchangia katika kupatikana kwa suluhisho la kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kilimo sehemu muhimu ya mazingira

Wito huo wa kuwekeza moja kwa moja kwa sekta ya kilimo kama mojawapo ya mikakati muhimu ya kufikia malengo ya makubaliano ya kuyaokoa mazingira yaliyofikiwa mwaka 2015 mjini Paris, Ufaransa ambayo yanawiana na ajenda ya 2030 ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu ulitolewa wakati wa kikao cha Ijumaa, tarehe 10 Oktoba cha siku ya kuchukua hatua katika sekta ya kilimo katika mkutano wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi wa Bonn ujulikanao COP 23.

Christian Schmidt Bundeslandwirtschaftsminister
Waziri wa chakula na kilimo wa Ujerumani Christian SchmidtPicha: picture-alliance/dpa/J. Carstensen

Mkutano huo ulikuwa unafuatilia hatua zilizofikiwa katika sekta hiyo ya kilimo tangu wadau kufikiana kuhusu hatua shirikishi za nyanja ya kimataifa katika mkutano uliopita wa mazingira uliofanyika Marrakesh.

Niabu wa mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO Rene Castro amesema nchi sasa zina fursa ya kuboresha sekta zao kilimo ili kuweza kuwa na usalama wa chakula kupitia kilimo endelevu na kuwepo mikakati ya kumiarisha matumizi mazuri ya raslimai, kuhifadhi mazingira na kuimarisha nyanja ya bio anuai na mali asili ili kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kuhusu sekta ya mifugo, Shirika la FAO linakadiria kuwa uchafuzi wa mazingira unaweza kupunguzwa kwa karibu asilimia 30 iwapo nchi zitatumia mbinu bora za ufugaji. Athari za mabadiliko ya tabia nchi zinawaathiri pakubwa wakulima, wafugaji, wavuvi na watu wa jamii zinazoishi misituni.

Ufugaji pia waaangaziwa COP23

Kuyasaidia makundi haya kwa kutumia suluhisho za ubunifu kutapunguza kutolewa kwa gesi chafu na pia kuzilinda jamii hizo na hivyo nchi pia zitaweza wakati huo huo, kufikia nyingi ya malengo yake yaliyomo katika ajenda ya maendeleoo endelevu.

DW eco@africa
Mfugaji wa ng'ombe wa maziwa nchini CameroonPicha: DW

Mawazo mbali mbali yalitolewa katika kikao hicho cha suluhisho zinazoweza kusaidia katika kuboresha kilimo na ufugaji katika mkutano wa COP23 ambao uliwajumuisha wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia, sekta ya kibinafsi, makundi ya wakulima wadogo na wanasayansi.

Miongoni mwa yaliyofikiwa ni kuongeza kiwango cha ufadhili wa kifedha katika sekta ya kilimo kutoka kwa sekta ya kibinafsi na ya umma, kutafuta wshirika zaidi watakaowasaidia wakulima,, wafugaji na wavuvi kufikia malengo yao, kuwaleta pamoja wadau kujadili kwa undani sera zinazohusu sekta hiyo na kuwekeza zaidi katika taarifa inayotolewa kwa wakulima na wafugaji kuhusu mbinu mpya za kilimo, hatari zilizopo, athari za uchafuzi wa mazingira na hatua za kuchukuliwa kuyaokoa.

Mwandishi: Caro Robi/https://cop23.unfccc.int/news/climate-action-investment-needs-to-move-faster-to-farming

Mhariri:Josephat Charo