1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Merkel na Macron mstari wa mbele kuyalinda mazingira

Caro Robi
14 Novemba 2017

Mashirika yasiyo ya serikali ya Ufaransa na Ujerumani yamewatolea wito Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuongoza mchakato wa kuharakisha malengo ya kuhusu kuyalinda mazingira.

https://p.dw.com/p/2nba7
Deutschland Frankfurter Buchmesse 2017 Merkel und Macron vor Eröffnung
Picha: Reuters/R. Orlowski

Merkel na Macron wanatarajiwa Jumatano kuhudhuria mkutano wa kimataifa unaojadili mabadiliko ya tabia nchi hapa mjini Bonn. Viongozi hao wawili wanaonekana kuwa manahodha wa mchakato wa kutekeleza malengo yaliyofikiwa katika makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza nchi yake inajiondoa kutoka makubaliano hayo.

Wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya serikali wamesema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili nchi ziweze kufikia malengo yao ya muda mfupi ya kupunguza viwango vya joto duniani kwa kupunguza gesi chafu ya Carbon ifikapo mwaka 2020.

Suala hilo limekuwa mojawapao ya masuala tete katika mazungumzo hayo ya mazingira yanayoendelea Bonn yajulikanayo COP23. Neil Makaroff mshauri wa mtandao wa Ufaransa kuhusu mabadiliko ya tabia amesema wangependa kuwaona Merkel na Macron wakishirikiana zaidi kuhusu suala la kuyahifadhi mazingira.

Ujerumani na Ufaransa zishirikiane kuhusu mazingira

Christian Averbeck mkurugenzi mkuu wa muungano wa mashirika ya mazingira Ujerumani amesema wanafurahishwa na kuwa Ujerumani na Ufaransa zinashirikiana na wangewahimiza viongozi wa nchi hizo kufanya uchumi wa nchi zao kuwa ule usiotoa gesi ya Carbon.

Hanoi Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/Kham

Aidha wametaka hotuba za Merkel na Macron zituame kuhusu hilo sio tu katika ngazi ya kitaifa, bali katika ngazi ya ushirikiano wa nchi hizo mbili na pia watumie nafasi yao barani Ulaya kama wenye nguvu zaidi kiuchumi kuyasogesha mbele malengo ya kuyalinda mazingira katika Umoja wa Ulaya.

David Banks, mshauri mkuu wa Rais Donald Trump kuhusu mabadiliko ya tabia nchi amesema licha ya kuwa Trump anakusudia kujiondoa kutoka makubaliano ya Paris, hiyo haimaanishi kuwa Marekani inaashiria kuwa nishati ya makaa na mafuta ndiyo njia pekee.

Banks alikuwa miongoni mwa ujumbe wa Marekani katika mkutano wa COP23 unaojadili ni vipi Marekani inaweza kusalia kuwa mstari wa mbele katika kupunguza gesi chafu na kuzisaidia nchi zinazoendelea kufikia malengo yao.

Wajumbe kutoka karibu nchi 200 wamekuwa wakikutana hapa Bonn kujadili namna ya kutekeleza vipengele vya makubaliano ya Paris yanayolenga kupunguza viwango vya joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili ili kuepukana na majanga kama vimbunga, mafuriko, ukame na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari.

Mwandishi: Caro Robi/unfcc/Reuters

Mhariri:Josephat Charo