1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Kiwango cha gesi ya Carbon sharti kipunguzwe

Caro Robi
14 Novemba 2017

Wataalamu wa mazingira wanaonya iwapo kiwango cha gesi chafu ya Carbon kitazidi kuongezeka kupita mwaka 2020 au kusalia katika viwango vya sasa, basi malengo yaliyowekwa katika makubaliano ya Paris hayataweza kufikiwa.

https://p.dw.com/p/2naVZ
Deutschland Weltklimakonferenz in Bonn - Proteste
Picha: Reuters/A. Doyle

Jopo la wataalamu wa mazingira leo litatoa muongozo wa ni kasi gani na kiwango gani cha gesi ya carbon inahitaji kupunguzwa ili kufikia malengo ya makubaliano ya Paris na pia wataelezea njia tofauti tofauti zitakaziosaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

Zaidi ya wanasayansi 15,000 wanaonya kuwa kuongezeka kwa gesi ya carbon, ukuaji mkubwa wa idadi ya watu duniani na mfumo wa maisha unaotumia kiasi kikubwa cha mali asili kuna athiri pakubwa dunia na kuharibu raslimali zake.

Wanasayansi hao wakiongozwa na Corine Le Quere aliyeongoza utafiti huo, wameendelea kuonya kuwa watu wanavuruga maisha yao ya baadaye na inatia wasiwasi kuwa ulimwengu unaendelea kuteleza kwa njia itakayosababisha majanga makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, mkondo unaosemekana kuwa mbaya zaidi kutishia kuangamia kwa viumbe hai katika kipindi cha miaka milioni 540.

Wakati wa kuchukua hatua ni sasa

Kundi jingine la wanasayansi nalo limetahadharisha kuwa viwango vya joto ambavyo vimepindukia nyuzi 1.1 vitasababisha barafu kuyeyuka katika ncha ya Antaktiki na hivyo kuongeza kina cha maji ya bahari hadi mita sita au saba zaidi na huenda ikachukua miaka mingine 1,000 kurekebisha mambo, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa sasa hivi kuyaokoa mazingira.

Symbolbild Australien Emissionssteuer
Moshi mchafu kutoka kiwanda cha SydneyPicha: AP

Wajumbe katika mkutano wa kimataifa wa mazingira unaondelea kwa wiki ya pili hapa Bonn wamesema mageuzi makubwa ya teknolojia mpya katika sekta ya viwanda yatachangia pakubwa katika kuusukuma mbele mchakato wa kuyalinda mazingira lakini hilo linaweza tu kufikiwa iwapo sekta ya biashara na serikali zitaunga mkono mageuzi hayo kupitia sera madhubuti na mikakati kabambe.

Asasi za kiraia pia zimetaka sekta ya kibinafasi kushirikishwa zaidi katika kampeini ya dunia ya kuyaokoa mazingira kwa kupunguza viwango vya joto kupitia kupuguza utegemezi wa nishati kama mafuta na makaa ya mawe.

Sekta hiyo ya kibinafsi imetakiwa kuwekeza zaidi, kuimarisha matumizi ya teknolojia mpya, na kuwa mstari wa mbele katika azma ya kupatikana suluhisho.

Leo vile vile, katika mojawapo ya vikao vya mkutano huo wa mazingira ujulikanao COP23, wanawake kutoka mataifa mbali mbali wataelezea mchango wao katika kuhakikisha ulimwengu ni mahali salama wakati juhudi za pamoja zinachukuliwa kuimarisha mazingira.

Hapo kesho, takriban viongozi wa nchi 30 wakiongozwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, na Rais Frank Walter Steinmeir watahudhuria mkutano huu wa mazingira ambao utakamilika siku ya Ijumma. Viongozi wengine wanaotarajiwa kuhutubia ni Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron,waziri mkuu wa Fiji Frank Bainimarama na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Mwandishi: Caro Robi/unfcc/AFP

Mhariri;Josephat Charo