1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP23: Hatua za dharura zahitajika kuyaokoa mazingira

Caro Robi
16 Novemba 2017

Shughuli zapamba moto, siku moja kabla ya mkutano wa kimataifa wa mazingira kufikia ukingoni Ijumma (17.11.2017) kwa kupatikana muafaka wa namna ya kuyaokoa mazingira.

https://p.dw.com/p/2njSl
UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Viongozi wa nchi, mawaziri, wanasiasa, wanaharakati wa mazingira, mashirika yasiyokuwa ya serikali na asasi za kiraia wako katika mchaka mchaka wa kujadili jinsi gani makubaliano ya kuyalinda mazingira ya Paris yatakavyotekelezwa ikiwemo ni namna gani nchi masikini zinaweza kusaidiwa ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi ili ifikapo kesho ambayo ni siku ya mwisho ya mkutano wa mazingira wawe wamefikia muafaka. 

Majadiliano yamepamba moto hapa Bonn, ikiwa ni siku moja kabla ya mkutano wa kujadili mabadiliko ya tabia nchi ujulikanao COP 23 kukamilika. Hayo yanakuja baada ya hapo jana viongozi wa nchi wakiongozwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuahidi kupunguza matumizi ya makaa ya mawe ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Macron alizitaka nchi zote kuharakisha mchakato wa kuhamia katika nishati jadidifu ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kusaidia kupunguza athari ambayo inaletwa na hatua ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa akizihimiza nchi za Ulaya kuwekeza zaidi kifedha katika mfuko wa hazina ya mazingira wa Umoja wa Mataifa ujulikanao IPCC ambao unakabiliwa na nakisi katika bajeti yake.

Kutokuwepo kwa Marekani kuna athari

Marekani imepunguza mchango wake wa dola milioni mbili kwa mwaka kwa mfuko huo, ambayo ilikuwa inachangia karibu nusu ya bajeti ya IPCC, ambalo ni jopo la maelfu ya wataalamu wa mazingira walio na jukumu la kufanya utafiti na kutoa ripoti za kisayansi kuhusu viwango vya joto duniani.

UN-Klimakonferenz 2017 in Bonn | Protest Gabun Diktatur
Waandamanaji nje ya ukumbi wa COP23Picha: DW/F. Görner

Wanaharakati wa mazingira wanasisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa na ni suala la dharura kufikiwa kwa malengo ya makubaliano ya Paris yaliyofikiwa mwaka 2015 angalau kwa kuweka malengo ya muda mfupi ambao ni mpaka mwaka 2020 kushuhudia kupungua kwa viwango vya joto duniani. Makubaliano hayo ya Paris yalifikiwa baada ya mazungumzo ya miongo miwili.

Leo asubuhi, kundi la watu limeandamana nje ya ukumbi wa mkutano huo wa COP23 kuwashinikiza viongozi kuchukua hatua madhubuti kuyaokoa mazingira na kusonga kutoka hatua ya ahadi hadi ya utekelezaji.

Nchi zilizoendelea kiviwanda zinashutumiwa kwa kujikokota kufikia maamuzi magumu ya kuondoka kutoka matumizi ya nishati za makaa ya mawe, mafuta na gesi hadi nishati jadidifu na pia kujitolea zaidi katika kuzisaidia nchi zinazoendelea kifedha ili kuweza nazo kufikia malengo yao ya kuyaokoa mazingira kuambatana na malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Wakati huo huo, watafiti kuhusu kuhusu usalama wa chakula wanaonya kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi kama ukame, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari huenda zikakasababisha baa kubwa la njaa duniani na kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaoukumbwa na utapia mlo ifikapo mwaka 2050.

Mwandishi: Caro Robi/unfcc/afp

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman