Conservatives yapoteza ngome muhimu uchaguzi wa Uingereza
6 Mei 2022Kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi ambayo yametangazwa siku ya Ijumaa. Matokeo hayo huenda yakaongeza shinikizo kwa Waziri Mkuu Boris Johnson katikati mwa kashfa za kimaadili na hali mbaya ya kiuchumi.
Uchaguzi huo uliofanyika siku ya Alhamisi kwa mabaraza zaidi ya 200 ulikuwa unachukuliwa kama kipimo cha maoni ya umma kuelekea uchaguzi mkuu ujao, ambao utafanyika mwaka 2024. Chama kikuu cha upinzani cha Labour ambacho kimekuwa nje ya madaraka ya kitaifa tangu mwaka 2010, kimeshinda udhibiti wa wilaya tatu za London za Wandsworth, Barnet na Westminster, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishikiliwa na chama cha Conservative.
Chama cha Johnson pia kimepoteza uungwaji mkono kwa chama cha Liberal Democrats kusini mwa Uingereza ambako chama cha Conservatives kilikuwa na ushawishi. Wapiga kura wengi wa tabaka la kati katika eneo hilo wanapinga Brexit na wamesikitishwa na kashfa ya kukiuka vizuizi vya Covid-19 na madai ya utovu wa nidhamu ya kingono yanayomzunguka Johnson na wanachama wengine waandamizi wa Conservatives.
Wakati matokeo ya karibu nusu ya England yakiwa yametangazwa kufikia Ijumaa, chama cha Labour hakikuwa kimepata ushindi mkubwa nje ya mji mkuu, hususan miongoni mwa tabaka la wafanyakazi kaskazini mwa England, maeneo ambayo Johnson alifanikiwa kushinda katika uchaguzi wa 2019 na kutoa ahadi ya kuboresha uchumi hasa baada ya Uingereza kujiondoa umoja wa Ulaya.
Mwenyekiti wa chama cha Conservatives Oliver Dowden amekiri kuwa matokeo jijini London yalikuwa "magumu" lakini akasema "picha zaidi tofauti" kwingineko zinaonyesha kwamba chama cha Labour hakijakuwa na nguvu ya kushinda uchaguzi mkuu.
Mratibu wa kitaifa wa kampeni wa Labour Shabana Mahmood, amesema matokeo hayo yanadhihirisha kwamba chama chao kinajenga msingi thabiti wa kurejea madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu mara nne. "Labour inapiga hatua ... ikichukua nafasi muhimu ya mabaraza ya Conservatives na kushinda katika majimbo muhimu ya Bunge kote nchini''.
Kiongozi wa chama cha Labour Keir Starmer amesema "tumeleta mabadiliko ndani ya Labour na sasa tunashuhudia matokeo yake".
Matokeo zaidi yatazidi kutolewa siku ya Ijumaa kutoka kote England na Scotland pamoja na Wales. Huko Ireland ya Kaskazini, wapiga kura wanachagua bunge la viti 90, huku kura za maoni zikionyesha kwamba Chama cha kitaifa cha kizalendo cha Sinn Fein huenda kikapata wingi wa viti bungeni na kushika nafasi ya waziri mkuu, na hivyo kuandika historia.
Kampeni za uchaguzi zilitawaliwa na kuongezeka bei za vyakula na mafuta, ambazo zimepelekea gharama za kaya kupanda. Vyama vya upinzani vinaitaka serikali kuweka jizihada zaidi ili kupunguza hali mbaya ya gharama za maisha inayochochewa na vita nchini Ukraine na janga la COVID-19 sambamba na athari za Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.