Conservative waanza mbio za kumsaka mrithi wa Truss
21 Oktoba 2022Chama hicho kitapaswa kumchagua kiongozi mpya kabla ya taarifa ya fedha kuwasilishwa mwishoni mwa mwezi huu.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Rishi Sunak na mtangulizi wa Truss, Boris Johnson. Gazeti la The Times, limeripoti kwamba Johnson anakusudia kujiunga katika kinyanganyiro hicho akiamini kwamba ni katika "maslahi ya taifa". Tayari wafuasi wake wameanzisha kampeni ya kutaka "kurejeshwa kwa Boris" huku wakosoaji wakiitaja hatua hiyo kama "tusi" kwa waingereza.
Mbunge mmoja ndani ya chama hicho Brendan Clarke-Smith katka mahojiano na kituo cha Sky News amesema kwamba waziri mkuu ajaye wa Uingereza anahitaji "mamlaka" kutoka kwa wapiga kura na wanachama, na kumpigia upatu Johnson kama mwanasiasa aliye na vigezo vyote. Mbunge mwingine Roger Gale, akielezea mpasuko ndani ya chama hicho, alisema kwamba Johnson anapaswa kuzuiwa kuwania tena, ikizingatiwa kuwa bado yuko chini ya uchunguzi wa bunge kuhusu kashfa ya "partygate" iliyomwangusha. "Hadi uchunguzi utakapokamilika na asikutwe na hatia, hakupaswi kuwa na uwezekano wa yeye kurejea serikalini".
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour Keir Starmer amerejelea mtizamo wake kwamba Johnson "hafai" kuongoza serikali.
Wakati huohuo viongozi mbalimbali wa nchi za magharibi wameelezea matumaini ya kurejea kwa utulivu kufuatia kujiuzulu kwa waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss, huku Urusi ikitoa ukosoaji mkali juu ya utawala wake mfupi.
Rais wa Marekani Joe Biden amesema kuwa ana matumaini Washington itaendelea kushirikiana kwa karibu na London, na kumshukuru Bi. Truss kwa ushirikiano wake katika masuala kadha ikiwemo kuiwajibisha Urusi dhidi ya vita vyake nchini Ukraine.
"Tutaendeleza ushirikiano wetu wa karibu na serikali ya Uingereza tunapofanya kazi pamoja ili kukabiliana na changamoto za kimataifa ambazo mataifa yetu yanakabiliana nayo."Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss ajiuzulu
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ana imani Uingereza itarejea haraka katika hali yake ya kawaida. "Nataka kusema kwamba Ufaransa, kama taifa na watu ambao ni marafiki wa watu wa Uingereza, inawatakia zaidi utulivu," alisema Macron, akisisitiza juu ya muktadha wa vita vya Ukraine na mgogoro wa bei ya nishati.
Waziri mkuu wa Ireland Micheal Martin amesema kwamba kuwa Ireland inataka kuona mrithi wa Truss akichaguliwa haraka iwezekanavyo ili "utulivu urejee kutokana na masuala muhimu ya kijiografia yanayoikabili Ulaya" ikiwemo vita vya Ukraine.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba Uingereza "Uingereza haijawahi kujua aibu kama hiyo kama waziri mkuu," kufuatia anguko la Truss.Uingereza: Mivutano yazidi kuudidimiza uongozi wa Waziri Mkuu Liz Truss
Itakumbukwa kuwa uhusiano kati ya Moscow na London umezorota kwa miaka kadhaa, kutokana na masuala kama vile kulishwa sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi mwaka 2018. Uhusiano baina ya nchi hizo mbili umedhoofika zaidi tangu mashambulizi ya Moscow nchini Ukraine. Uingereza ni moja ya washirika wa Kyiv na Urusi inaichukulia kama mojawapo ya nchi za Magharibi ambazo si rafiki. Truss alitembelea Urusi kama waziri wa mambo ya nje mnamo Februari, wiki mbili tu kabla ya Rais Vladimir Putin kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine.