Congo yaanzisha tena mazungumzo na vyama vya waalimu
29 Oktoba 2021Mashambulizi ya maneno yameshuhudiwa Ijumaa ya leo kwenye hoteli ya Mbuela Lodge mjini Kisantu mkoa wa kati ya Jamhuri ya Kimemokrasia ya Kongo kunakofanyika majadiliano hayo kati ya Tume ya pamoja inayo jumuisha viongozi wa kiserikali na wasimamizi wa miungano mbalimbali ya walimu.
Tangu jana jioni, Waziri wa Elimu Tony Mwaba Kazadi ameendelea bila kuchoka kuwasihi walimu kusitisha mgomo wao na kurudi shuleni haraka iwezekanavyo ili kuokoa mwenendo mzuri ratiba ya masomo kwa mwaka wa shule.
"Chini ya uongozi wa Rais Félix Tshisekedi Tshilombo, serikali ya Sama Lukonde imedhamiria kwa dhati kutekeleza sera ya elimu ya msingi bila malipo ili kuwaruhusu watoto wetu sio tu kwenda shule tu, bali pia na zaidi ya yote kufaidika na elimu bora. Ndio maana serikali inashiriki katika mazungumzo ya kudumu na wawakilishi wa walimu wetu ili tupate suluhisho. Kwa hili, tunaomba miungano ya walimu ituhakikishie leo ikiwa hivi karibuni masomo shuleni yataendelea kama kawaida.",alisema Mwaba.
Soma pia:Maandamano ya upinzani nchini Congo yatawanywa na polisi
''Waalimu wanataka vitendo na sio maneno''
Pia Waziri Tony Mwaba amejitetea kwa marefu kuhusu nia ya serikali ya kutaka mambo yaboreshwe, akihakikisha pia kuwa walimu ambao walikuwa wamesitishwa kazi wamerudishwa kwenye orodha ya malipo tangu Oktoba 27.Hata hivyo, wawakilishi wa walimu wanazidi kusisitiza madai yao ya kuboreshewa mshahara.
Wakati huo, Naibu Waziri Mkuu akiwa pia Waziri wa Utumishi wa Umma Jean-Pierre Lihau anayeshiriki pia kwenye majadiliano hayo amekumbusha kuwa elimu imekuwa dharura ya kitaifa na moja ya vipaumbele kwa watoto ambao wanaunda mustakabali wa kesho nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akionya walimu kuwajibika. Majadiliano hayo bado mwishoni mwa wiki hii.