Confederations Cup ; Brazil na Japan wafungua dimba
14 Juni 2013Brazil imekamilisha matayarisho kwa ajili ya kombe la mabara , Confederations Cup licha ya kazi za dakika za mwisho zikiwa bado zinaendelea katika baadhi ya viwanja vitakavyopigiwa mtanange huo kuanzia leo hadi tarehe 30 mwezi huu. Wenyeji Brazil wanafungua dimba na Japan jioni ya leo.
Rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Sepp Blatter pamoja na watayarishaji wa mashindano hayo wamesema wiki hii.
Hainishangazi kuona kuwa bado baadhi ya kazi za ujenzi zinaendelea . Kutakuwa na mengi yatakayotokea katika dakika za mwisho, Blatter amewaambia waandishi habari mjini Rio de Janeiro.
"Kila kitu kitakuwa tayari kwa wakati. Tunafahamu kuwa sio kila kitu kiko kamili kabisa. Lakini kuwa kamili si jambo la lazima, lakini kila kitu kitakuwa tayari muda ukifika. Na kwa hilo nina uhakika."
Nae katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke ameongeza kuwa hakuna haja ya kufananisha maandalizi ya mashindano kama haya yaliyofanyika nchini Afrika kusini na mwaka huu nchini Brazil.
"Hakuna sababu ya kufananisha Afrika kusini na Brazil. Ni kwamba tunafurahishwa mno , na shauku ya Wabrazil katika soka na sio tu kwa upande wa timu yao ya Brazil , lakini ni kwa timu zote na michuano hii kwa jumla."
Je Brazil inaweza?
Mashindano hayo yanayoanza leo(15.06.2013) hadi Juni 30 ni mtihani mkubwa kwa Brazil kuonyesha uwezo wake wa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa kama ya kombe la dunia mwakani. Sita kati ya viwanja 12 vya fainali za kombe la dunia vitatumika , na fainali itafanyika katika uwanja uliofanyiwa ukarabati na uliofunguliwa hivi karibuni wa Maracana mjini Rio.
Huenda pia teknolojia ya kuonesha kuwa bao limeingia ikatumika kwa majaribio katika michuano hiyo ya Confederations Cup kwa mara ya kwanza . Kiongozi wa kampuni ya Ujerumani ya GoalControl Dirk Broichhausen ana matumaini kuwa mivutano ya kudai kuwa goli limeingia ama la itatupwa katika kapu la historia ya soka.
Pamoja na hayo Broichhausen anasisitiza kuwa ana wasi wasi na utengaji. Hata hivyo anamatumaini ya kufanya majaribio halisi ya mfumo huo. Itakuwa jambo zuri sana , iwapo utaweza kuwa wa manufaa kwa mchezo huu.
Green Eagles yaanza vurumai
Nigeria , Green Eagles mwakilishi wa bara la Afrika katika mashindano haya ambayo ilibakia nchini Namibia baada ya pambano lao la kufuzu katika fainali za kombe la dunia kutokana na mzozo wa malipo ya bonasi , walichelewesha kuondoka kwao kwenda katika michuano ya Confederations Cup nchini Brazil. Nigeria hata hivyo inakwenda Brazil baada ya kufuta mgomo wa wachezaji hali ambayo ingeathiri mashindano hayo.
Na katika hatua ya wachezaji kuhamia katika vilabu vingine barani Ulaya , Cristiano Ronaldo wa Real Madrid ameonyesha zaidi hali ya kutaka kuihama klabu hiyo wiki hii baada ya kusema hajamwaga wino kwa mkataba mpya na timu yake hiyo. "Taarifa zote za kwamba nimetia saini mkataba mpya na Real ni uongo." Ronaldo ameandika katika ukurasa wake wa Tweeter bila kutoa maelezo zaidi.
Mkataba wa sasa wa Mreno huyo unamalizika mwaka 2015. Seville ya uhispania imepata saini ya mshambuliaji Raul Rusescu kutoka Romania kwa mkataba wa miaka mitano kufuatia kuondoka kwa winga Jesus Navas ambaye anajiunga na Manchester City msimu ujao. Seville imekubali kumruhusu Navas kujiunga na City wiki hii na mshambuliaji mwingine wa klabu hiyo Alvaro Negredo anahusishwa pia na kuihama klabu hiyo.
Liverpool ya Uingereza inajiwinda kukiimarisha kikosi chake kwa kumpa mkataba Iago aspas kutoka Celta Vigo ya Uhispania .
Na klabu ya Malaga ya Uhispania itapata huduma ya kocha Bernd Schuster msimu ujao kwa muda wa miaka mitano . Schuster raia wa Ujerumani anachukua nafasi inayoachwa wazi na Manuel Pellegrini, ambaye amejiunga na Manchester City msimu ujao baada ya Mtaliani Roberto Mancini kufutwa kazi.
Gareth Bale ambaye anasemekana kuwa ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu kabisa katika historia ya wachezaji wa Uingereza amehusishwa na kuhamia vilabu mbali mbali msimu huu. Lakini taarifa ambazo si rasmi zinasema sasa mchezaji huyo anawaniwa na mabingwa wa Premier League Manchester United.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae /rtre / ape
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman